Wednesday, 29 July 2015

Dk. Benson Bana.
Uamuzi wa jana wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kujitoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na Chama cha Demokrasia na maendeleo (Chadema), wananchi kadhaa wametoa maoni tofauti kuhusiana na uamuzi wa mwanasiasa huyo.
 
MAKAMU RAIS TEC
Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Mhashamu Severine Niwemugizi, alisema hatua ya Lowassa ni ukomavu wa vyama vya siasa nchini hasa vya upinzani kuwa mtu yoyote anaweza kuhama na kujiunga na chama chochote.
 
Alisema kuhama kwa Lowassa kunatafsiri kuwa mchakato wa uteuzi ndani ya CCM haukumridhisha.
 
“Tafsiri ni kuwa ameona CCM haikumtendea haki na kama binadamu yeyote ana haki ya kuchukua hatua kama binadamu mwingine, mtu anapoona hajatendewa haki kama binadamu uamuzi ni wake kuondoka kama wengine wanavyobadilisha vyama, hatushangai ni jambo linatokea kwa wengi siyo la pekee sana,” alisema na kuongeza:

CCM yaonya vijana kubeza wagombea wake.


Chama Cha Mapinduzi (CCM)
Katibu Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Songea Mjini mkoani Ruvuma, Marco Mbawala, amewaonya baadhi ya vijana wanaosadikiwa kuwa wanachama wa vyama vya upinzani  kuacha kuwakejeli wagombea ubunge wa Jimbo la Songea mjini kwa tiketi ya CCM ili kuepusha vurugu na kuharibu mchakato wa uchaguzi ndani ya chama hicho.
 
Onyo hilo alilitoa juzi baada ya baadhi ya vijana hao kuwauliza maswali ya kejeli wagombea ubunge hao, wakati wakijinadi kwenye mikutano ya chama hicho katika kata za Mshangano, Msamala na Bombambili.
 
Marko alisema wagombea hao wanaomba ridhaa kwa wanaCCM  ili apatikane mmoja wao wa kupeperusha bendera ya chama hicho katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika nchini Oktoba 25, mwaka huu.
 
Alisema wanachama wa vyama vingine hawana ruhusa ya kuwauliza maswali wagombea wa CCM bali wasubiri atakapopatikana wa kupambana na atakayechaguliwa kutoka vyama vingine vya upinzani.
Vilevile  katibu huyo amewataka wanachama wa chama hicho kuacha tabia za kuuliza maswali ya kupandikizwa wagombea hao bali wafanye hivyo kwa kwa utashi wao.
 
Wagombea hao ni Leonidas Gama (Mkuu wa mkoa Kirimanjaro), Francis Miti (Mkuu wa Wilaya ya Hanang’  mkoani Arusha), Theresia Uvisa ambaye (alikuwa mbunge viti maalum kupitia vyuo vikuu vishiriki na Waziri wa Mazingira),  Azizi Mohamed (Katibu wa CCM Namtumbo), Sebastian Waliyuba (Wakili wa kujitegemea).
 
Wengine ni Erick Mapunda (Mhadhiri wa Chuo kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya) ,Raymond  Mhenga (Ofisa Masoko wa Claus FM) na  Mussa Gama ambaye ni mtoto wa Marehemu Lawrence Gama (Katibu Mstaafu wa CCM ). 

Tuesday, 28 July 2015

“Watanzania wanataka mabadiliko...watayatafuta nje ya CCM"




Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere


Dar es Salaam. Kauli ya hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kuwa Watanzania wanataka mabadiliko na wasipoyapata ndani ya CCM, watayatafuta nje ya CCM inaweza kutimia mwaka huu.

Lowassa sasa rasmi Ukawa,muda wowote kutangazwa mgombea urais

Lowassa aliondoka hotelini hapo  baada ya kukaa kikaoni kwa saa 1.38 (dakika 98).  Aliagwa na viongozi mbalimbali wa Chadema. 

Dar es Salaam. Katika dakika za mwishomwisho wakati wa mchakato wa kuwania urais kwa tiketi ya CCM, habari za mmoja wa wagombea aliyekuwa na nguvu katika kinyang’anyiro hicho, Edward Lowassa kwamba angeenguliwa zilivuma mno na kuibua swali la atakatwa hakatwi?

Thursday, 9 July 2015

Maoni juu ya Burundi: wakati wa kuchukua hatua ni sasa

Serikali ya Burundi imeshinda uchaguzi wa Bunge.Lakini uchaguzi huo ulikuwa hadaa. Siku chache kabla ya uchaguzi wa Rais nchini humo hatari ya kuzuka vita vingine vya wenyewe kwa wenyewe imezidi kuwa kubwa .

Vijana wa Imbonerakure wawaweka watu roho juu
Vijana wa Imbonerakure wawaweka watu roho juu
Matokeo ya uchaguzi wa Bunge nchini Burundi hayakumshangaza yeyote. Uchaguzi huo haukuwa huru wala wa haki. Kwani, ulifanyika bila ya usimamizi wa tume huru ya uchaguzi na bila ya waangalizi huru.

Vituo vitatu vya televisheni vyatozwa faini, vyaony

Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Prof. John Nkoma.
Vituo vitatu vya televisheni vimetozwa faini na kupewa onyo kwa kurusha taarifa zilizokiuka kanuni  za huduma ya utangajaji.
 
Vituo hivyo ni Chanel Ten kupitia kipindi chake cha Kanjanja Time kimepewa onyo na kutozwa faini ya Sh. milioni 2.5, Star Tv kupitia kipindi chake cha Min Buzz  kimepewa onyo na faini ya Sh. 500, 000 na Tanzania Broadcasting Corporation (TBC1) onyo na faini ya Sh. 500, 000 kwenye mojawapo wa taarifa za habari zilizorushwa na kituo hicho.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana,  Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Margeret Munyangi,  alisema wameamua kuchukua hatua hizo baada ya kamati hiyo kukaa na kujadili ukiukwaji wa kanuni za utangazaji za mwaka 2005.
 
Alisema Mei 30, mwaka huu,  kituo cha Chanel Ten kupitia kipindi cha Kanjanja Time kilichorushwa hewani kuanzia saa 2:45 hadi saa 3:10 usiku   taarifa iliyoonyesha picha ya mgonjwa akiwa katika wodi ya Hospitali ya Serikali mjini Songea huku sehemu ya makalio yake yakiwa wazi na kuonyesha vidonda.

Niyonzima: Nauguza, wakipona nitarudi.

Katibu Mkuu wa Yanga, Jonas Tiboroha.
Kiungo wa kimataifa wa Yanga kutoka Rwanda, Haruna Niyonzima 'Fabregas', amesema sababu inayomfanya achelewe kurejea nchini kujiunga na timu yake inayojiandaa na mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) ni kuuguliwa na watoto wake wadogo mapacha.
 
Akizungumza na gazeti hili juzi mchana kwa njia ya simu kutoka Kigali, Rwanda, Niyonzima alisema atarejea nchini mara tu hali ya watoto wake itakapokuwa vizuri.
 
Niyonzima alisema anafahamu majukumu yake ndani ya klabu na kinachomchelewesha kurejea nchini, ni kutekeleza majukumu yake kama baba wa familia.
 
"Nitarudi hivi karibuni Inshaallah, hivi tunavyoongea na wewe niko hospitali, nipigie baadaye tutaongea zaidi," alisema kwa kifupi Niyonzima alipozungumza na gazeti hili juzi Julai 7, mwaka huu saa 6:19 mchana kwa saa za Tanzania sawa na saa 5:19 kwa saa za Kigali, Rwanda.
 
Jana kiungo huyo hakuweza kupatikana tena katika simu yake ya mkononi inayoishia na namba ...719 kuelezea zaidi tatizo linalomchelewesha kurudi nchini  kushiriki kwenye mazoezi pamoja na wachezaji wenzake.

Majina yao kuanikwa leo, wengine 33 kufyekwa.


Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) leo inakutana kuchuja majina ya makada wake 38 waliorejesha fomu za kuomba kuteuliwa kuwania urais kupitia chama hicho na majina 33 ni lazima yapigwe panga ili kupeleka majina matano kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kupigiwa kura.
 
Kwa mujibu wa habari kutoka mitandao ya kijamii, kwenye vijiwe na mijadala sehemu mbalimbali, majina hayo matano yanaaminika kwamba yatatoka miongoni mwa watiania 10 ambao wametajwa zaidi katika mijadala hiyo.
 
Sababu kuu mbili ambazo zimekuwa zikitolewa kwenye mijadala hiyo na hata na baadhi ya wachambuzi wa mambo ya siasa Tanzania ni mbili. Mosi, uzoefu wao ndani ya ungozi wa serikali na pili, nafasi yao ndani ya chama, ama kama wajumbe wa NEC au Kamati Kuu.
 
Majina ambayo yanatazamiwa kwamba yanaweza kupenya Kamati Kuu ni pamoja na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal; Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; Waziri wa Sheria na Katiba, Dk. Asha-Rose Migiro; Waziri Mkuu Mizengo Pinda; Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Profesa Mark Mwandosya; Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani; Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye na Waziri wa Ujenzi, John Magufuli;.

Wednesday, 8 July 2015

Mkutano Mkuu wa CCM ukiendelea kwa Uchaguzi wa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti leo Dodoma


Mwenyekiti wa CCM Taifa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete akiondoka katika kiti cha Mwenyekiti baada ya kujiuzu na Makamu wake wa Zanzibar Dk. Amani Abeid Karume na Pius Msekwa wa Tanzania Bara ,wakiondoka katika sehemu hiyo na kukaa sehemu maalumu kwaajili ya kupiga kura.

Mwenyekiti wa Muda wa Uchaguzi wa kumchangua Mwenyekiti wa CCM, Rais Mstaaf wa Tanzania Benjamin Mkapa akiongoza kikao hicho katika muda wa kupiga kura.
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa  Tanzania Dk. Kikwete Mrisho Kikwete na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, wakiwa katika nafasi maalum baada ya Mwenyekiti kujiuzulu akiwa na viongozi wengine  wakati wa kupiga kura ya kumchagua Mwenyekiti na Makamu wa Zanzibar na Bara. 
Mama Maria Nyerere, Mama Fatma Karume, na wake wa Viongozi wengine wakiwa katika ukumbi wa Mkutano wakati wa uchaguzi ukiendelea jioni hii mjini Dodoma.
Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano Tanzania Dk. Mohammed Gharib Bilal, na Waziri Mkuu Mstaafu Msuya.wakibadilishana mawazo wakati wa mkutano mkuu wa CCM ukiendelea kwa hatua ya kumchagua Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Zanzibar na Bara, kulia Rais Mstaafu wa Zanzibar Dk. Salimin Amour Juma akiwa katika ukumbi wa mkutano Kizota mjini Dodoma

Matokeo ya chaguzi za nafasi 10 za wajumbe wa NEC -CCM Tanzania Bara wa Chama cha Mapinduzi zinazoendela Dodoma yametoka ni kama ifuatavyo:



1. Stephen Wassira - 2,135
2. January Makamba – 2,093
3. Mwigulu Nchemba – 1,967
4. Martine Shigela – 1,824
5. William Lukuvi – 1,805
6. Bernard Membe – 1,455
7. Mathayo David Mathayo – 1,414
8. Jackson Msome - 1,207
9. Wilson Mukama - 1,174
10. Fenela Mukangara - 984

Chadema yaonya watakaotumia fedha kusaka uongozi.


Mbunge wa Musoma Mjini (Chadema), Vicent Nyerere.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Mara,  kimewaonya wanachama wake wanaosaka uongozi waepuke kutumia fedha vinginevyo majina yao yatakatwa na kuchukuliwa hatua kulingana na taratibu za chama hicho.
 
Mbali na hilo, wametakiwa pia kuepuka kupakana matope kwenye kampeni ndani ya chama, kwa vile watakiwa wanakiharibia mbele ya wananchi ambao ndiyo wapigakura.
 
Mwenyekiti wa Chadema wa mkoa huo, Vicent Nyerere (pichani)  alitoa onyo hilo juzi, alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya Mukendo mjini Musoma.
 
Nyerere ambaye pia ni Mbunge wa Musoma Mjini (Chadema), alikuwa akihamasisha wakazi wa mji huo kuendelea kujitokeza kwa wingi kwa kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapigakura.
 
Alisema kipindi cha uchukuaji wa fomu za kuwania udiwani na ubunge kumekuwapo na taarifa kwamba baadhi ya wanaotaka kuwania nafasi hizo wamekuwa wakihusishwa na vitendo vya ugawaji fedha na kuharibiana wenyewe kwa wenyewe.
 
Alisema kuwa Chadema haina sifa za ulaji rushwa, hivyo atakayebainika kujihusisha na vitendo hivo, jina lake litakatwa mapema sana na kisha hatua nyingine zitachukuliwa dhidi yake.
 
"Hiki chama siyo cha wala rushwa, kama kweli kuna mtu anatumia fedha kuhonga wananchi ili apenye kwenye mchakato wa kupata mwakilishi kwenye ngazi ya kata na jimbo, basi ahesabu maumivu," alisema Nyerere.
 
Alisema  Chadema ni chama mbadala, hivyo hakina budi kufanya mambo ambayo yanalenga kuleta maendeleo na siyo kama vyama vingine ambavyo ulaji rushwa limekuwa ni jambo la kawaida.
 
"Nirudie kwamba kama kuna mtu anatumia fedha kuhonga ili apate uongozi, atambue kuwa Chadema hakina utaratibu, akatafute kwingine atawapa wanaoendekeza vitendo hivyo," alisema.
 
Mwenyekiti huyo alisema mtu anayetafuta uongozi kwa kuhonga hafai na anaweza kuwa mzigo kwa taifa.
 

Monday, 6 July 2015

Juhudi za kuhifadhi uoto wa asili na misitu Shinyanga

NGITILI ni eneo maalumu ambalo linatengwa kwa ajili ya kuhihadhi uoto wa asili na misitu. Hizi ni juhudi ambazo zinafanywa katika nchi za Afrika ili kuweza kukabiliana na tatizo la mabadiliko ya tabia nchi hasa ukame

Tansania Projekt Baumpflanzung Reduzierung Karbondioxid


Nchini Tanzania katika mkoa wa Shinyanga zaidi ya wakazi 50 wamefanikiwa kuhifadhi NGITILI baada ya mradi wa majaribio wa kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa unaotokana na ukataji miti hovyo na uharibifu wa misitu MKUHUMI kufanyika kwa majaribio kuanzia mwaka 2009 hadi 2014 unaotekelezwa kwa ubia kati ya Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) kuwapa elimu wananchi hao jinsi ya kuhifadhi NGITILI.
Mradi huo umeonekana kuwa na mafanikio baada ya NGITILI hizo kuonekana kufanikiwa kupunguza kiwango cha hewa ukaa angani.
Mpango wa kupunguza uzalishaji hewa ukaa unaotokana na ukataji miti hovyo na uharibifu wa misitu yaani MKUHUMI, umetekelezwa kwa majaribio kwa miaka mitano kuanzia mwaka 2009-mpaka mwaka 2014 na umetekelezwa kwa ubia kati ya Shirika la Kuhifadhi Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania yaani Mjumita. Miongoni mwa mikoa ambayo imetekeleza mradi huo wa majaribio nchini Tanzania ni mkoa wa Shinyanga ambapo moja kati ya utekelezaji wake ni uhifadhi wa NGITILI.

Ali Kiba:Tuzo za Kilimanjaro ni haki yangu



Msanii kutoka Tanzania Ali Kiba ambaye amejitokeza tena katika ulingo wa muziki baada ya kupumzika kwa miaka mitatu amepuuzilia mbali madai kwamba alipendelewa katika tamasha la tuzo za Kilimanjaro.
Ali kiba ambaye alipata tuzo sita na kumshinda msanii wa kimataifa Diamond Platinum amesema kamwe hakupendelewa na kwamba ni muziki wake unaopendwa na wengi.
Akizungumza katika mahojiano na runinga ya Citizen siku ya ijumaa usiku nchini Kenya,Kiba amesema kuwa anahisi yeye ndio bora na kwamba ilikuwa haki yake kushinda tuzo hizo.
''Nahisi kwamba mimi ndio bora na nilifaa kushinda tuzo hizi.''Mashabiki wangu waliukosa mziki wangu na ndio maana walinipigia kura na ndio maana nilishinda tuzo sita kati ya saba nilizoteuliwa'',alisema.
Na alipoulizwa kuhusu uhusiano wake na Diamond,Kiba alikana madai kwamba wawili hao hawana uhusiano mwema.
''Sina uadui wowote kati yangu na Diamond na haujakuwa''. Naweza kukuhakikishia kuwa mimi na Diamond hatujapigania kuhusu chochote''.
Hatahivyo amesema kuwa inamkera wakati watu wanapomlinganisha na mwimbaji huyo wa Mbagala.
Alisema:Mimi ni mimi na Diamond ni Diamond.

Kauli ya Mbunge Lusinde: Wananchi watoana ngeu.


Mbunge wa Mtera, Livingston Lusinde.

Mbunge wa Mtera, Livingston Lusinde, juzi alisababisha mapigano yaliyojeruhi wapigakura wake kadhaa.
Baadhi ya wapigakura wake kumzomea wakipinga hoja zake alizokuwa akitumia kujinadi katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Nkwenda wilayani Chamwino, mkoani Dodoma.
Mkutano uliondaliwa na serikali ya kijiji ili kumpa nafasi mbunge huyo kuzungumza na wananchi wake juu ya mambo mbalimbali ya maendeleo aliyoyafanya kwa taktibani miaka minne na nusu.
Alianza kwa kueleza alivyo tumia fedha kutekeleza miradi ya barabara, zahanati, maji pamoja na mambo mengine ambayo yote alisema imegharimu zaidi ya Sh. milioni 400 na vile vile kujinadi kuwa yeye ndiye alileta mradi wa Tasaf na fedha zinazotumika ni za kwake.
Baada ya mbunge kueleza hivyo, kundi la wananchi walianza kuzomea na kupiga kelele kuwa mbunge anadanganya kwa kuwa hakuna miradi ambayo imetekelezwa katika kijiji hicho kwa kiasi cha fedha hizo na za Tasaf ni za serikali sio zake. 
“Mbunge huyo ni uongo huwezi kutudunganya hakuna kitu kama hicho baaadhi ya sauti za wananchi zilisikika. Baadhi ya sauti hizo zilisema: ‘ 
“Mbunge hujafanya kitu, hii miradi sio wewe usindanye wananchi.”
Kutokana kelele hizo zilizodumu kwa zaidi ya dakika kumi na Lusinde kubaini hakuna ayemsikiliza, aliwaeleza wananchi kuwa wakae katika makundi mawili moja wanamuunga mkono na wasio muunga mkono. 
“Naomba wale ambao tupo pamoja wakae kulia na wale ambao hatuko pamoja wakae kushoto ili kutambuane kwa vizuri zaidi,” alisema Lusinde.
Baada ya makundi hayo wawili kujitenga huku idadi kubwa ya wanawake ili wale wanaomuunga mkono na wanaume kubaki upande usio muunga mkoano, Lusinde  aliwaamuru vijana wapatao 15 kuwashambulia watu wanaopingana naye. 
“Sasa nyinyi kama mnajifanya ‘masteling’ basi mimi ni steling zaidi yenu sasa makomando wangu watawashughulikia, sisi tuko tayari hata kufa,” alisema  Lusinde.
Baada ya kauli hiyo vijana hao walitoa fimbo na marungu na kuanza kuwashambulia wananchi na kusababisha watu wakaanza kukimbia ovyo na wengine kujificha majumbani kwa kujifungia milango kuhofia kipigo.
Mmoja wa majeruhi hao Yohana Mnyanyi, aliyeshonwa juzi saba,  lisema  alikuwa akitoka eneo ambalo walikuwa wakichimba kaburi akielekea nyumbani ndipo alipokuna na watu zaidi ya kumi wakiwa wamebeba fimbo na marungu wakikimbiza watu na kuwapiga.
“Mimi wakati nakuja nikakutano na watu wanakimbizana nikauliza kuwa jamii hii ni vita au kitu gani kabla sijamaliza nikapigwa fimbo nikakinga mkononi hapa nilipovimba, lakini pia nikapigwa ya pili kichwani hapa niliposhonwa nyuzi saba na kuaguka chini…lakini mbunge Lusinde naye alikuwepo akisema ngoja leo makomando wangu wafanye kazi yao tuheshimiane,” alisema Mnyanyi.
Saidi Elieza alisema pamoja na watu hao kutumia fimbo lakini pia mmoja wa waopambe wa Mbunge alikuwa ameshikilia panga akisema atayejifanya jeuri atamkata shingo yake.
Alisema kuwa mara baada ya vurugu hizo kuanza walianza kupigwa watu na cha kusikitisha zaidi hadi watu wenye matatizo ya akili walipigwa.
 Mganga wa Zahanati ya Kijiji Cha Nkwenda, Elisha Chizuwa, alithibitisha kupokea watu watatu na kuwa wawili kati yao moja alishonwa nyuzi saba, mwingine tano na mwingine alimpatia matibabu ambapo akiwa ameumia ubavuni.
“Nilipatiwa taarifa na ofisa Mtendaji wa Kijiji aliniambia kuwa watu hao wamejeruhiwa katika vurugu zilizotokea kwenye mkutano wa mbunge,” alisema.
 Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho Jonas Chitunga, pia alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo na kuiomba serikali kuongeza ulinzi wakati wa mikutano ya kisiasa.
Lusinde alipoulizwa alidai kuwa kuna watu waliokuwa wamenunuliwa pombe za kienyeji ili waharibu mkutano wake na kuwa waliwaomba watulie, lakini walikataa ndipo na wao wakaanza kuwapiga kwa kujihami.

Mbatia amshukia Spika Makinda.


Mbunge wa kuteuliwa na Mwenyekiti wa Chama cha NCCR- Mageuzi, James Mbatia.

Mbunge wa kuteuliwa na Mwenyekiti wa Chama cha NCCR- Mageuzi, James Mbatia,  amesema hakuna Spika aliyewahi kuonyesha udhaifu katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama alivyoonyesha Anna Makinda.
Amesema Makinda ameligawa vipande vipande Bunge la 10 na kutumiwa na mhimili wa utawala.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mbatia alisema badala ya Bunge kuisimamia serikali, lakini Makinda ameshindwa kuliongoza Bunge hilo kutokana na shinikizo la mhimili wa utawala na kulazimika kufuata matakwa ya CCM na hivyo kuliongoza kwa ubabe.
 
Alisema tofauti na ilivyokuwa katika kipindi cha  Samuel Sitta na Pius Msekwa ambao walionyesha weledi na kuliongezea heshima Bunge, lakini Makinda ameriharibu kutokana na kuacha kusimamia Katiba ya nchi katika kuliongoza Bunge hilo.
 
“Siku zote mwanamke ndiye huwa ni mtu wa mwisho kuligawa Taifa, lakini limekuwa ni jambo la ajabu sana kuona mwanamke huyo ambaye angekuwa mstari wa mbele katika kuitetea nchi hii, lakini ameamua lifie mikononi mwake, hata bila kuficha ameonyesha wazi kwamba anatumika na serikali na CCM, Makinda yeye siyo kiranja wa bunge  ni mratibu tu,” alisema Mbatia.
 
Aliongeza: “ Badala ya Bunge kusimamia serikali kama Mhimili unaojitegemea, limejivua kazi yake na kuwa kiungo cha serikali na inalisimamia, na ndiyo  maana hata juzi mlisikia Serikali inasema imeoliongezea Bunge siku, badala ya Bunge lijiongezee lenyewe, hii ni fedheha.”
 
Mbatia alisema suala la kupelekwa bungeni kwa hati ya dharura na kujadiliwa miswaada mitatu ya mafuta na gesi ni ajenda ya siri ya kutaka kuiweka gesi kama dhamana ya CCM ya kupata fedha ya uchaguzi na  kwamba hicho ni kiashiria cha kuanza kuiuza nchi rejareja.
 
“Raslimali hizi badala ya kuwa neema kwa Watanzania, sasa inakuwa balaa, watu wachache wanataka kuwaibia Watanzania, hivi unawezaje kuwekaje miswaada hii muhimu kujadiliwa kwa pamoja na kuipeleka harakaharaka hivyo, sisi tumesema hatukubali kuona hujuma hizi zinafanyika dhidi ya rasilimali na Taifa,” alisema Mbatia.
 
Mbatia alisema msimamo wa Wabunge wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) uko wazi, kwamba hawako tayari kujadiliwa miswaada hiyo kwa hati ya dharura na pia hawatashiriki wakati wa kuvunjwa bunge hilo Julai 9, mwaka huu.
Pia aliongeza kuwa hata wakiitwa katika meza ya maridhiano na Makinda hawatakuwa tayari kushiriki.
 
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alipoulizwa juu ya taarifa hizo za kwamba chama hicho kina  ajenga ya siri ya kuifanya gesi kusaidia kuwa dhamana  katika uchaguzi, alijibu kwa kifupi kwamba ni uzushi.
 

Sunday, 5 July 2015

Mbinu hii imefeli Spika, maridhiano kwanza


Spika wa Bunge, Anne Makinda

Jana, Spika Anne Makinda alilazimika kuahirisha shughuli za Bunge asubuhi baada ya wabunge wa vyama vya upinzani kupiga kelele na hivyo kusababisha muwasilishaji wa Muswada wa Sheria ya Mafuta na Gesi wa mwaka 2015 asisikike vizuri.

Dawa mpya ya ukimwi yakosolewa


Kwa muda mrefu wahudumu wa afya ya masuala ya ngono wamesisitiza matumizi ya mipira ya kondomu kama mbinu bora zaidi dhidi ya maambukizi ya virusi vya ukimwi.
Lakini tabia moja hatari ya kutumia madawa ya kulevya na wapenzi wa jinsia moja inazidi kuibua wasiwasi.
kumekuwa na njia nyingi za kinga dhidi ya virusi vya ukimwi, lakini kuna dawa moja mpya - Pre-Exposure Prophylaxis (PrEP) - ambayo inaweza kutoa kinga dhidi ya maambukizi ya ukimwi iwapo itatumika kabla ya kushiriki ngono.
Utafiti unaofanywa na daktari Sheena McCormack kutoka chuo kikuu cha London, unasema kwamba unapomeza dawa hiyo, inazuia maambukizi ya ukimwi kwa kuzuia ongezeko la virusi, hii ni baada ya majaribio kufanyiwa kundi moja la wapenzi wa jinsia moja, ambao wamo katika hatari kubwa zaidi ya maambukizi
Shirika la afya duniani limetambua kwamba dawa hiyo ya tembe inaweza kupunguza maambukizi kwa kiwango kikubwa.
Baadhi ya wakosoaji wanasema kuwa dawa ya aina hii inahamasisha watu wengi kushiriki ngono bila kutumia mipira ya kondomu
Hata hivyo matumizi ya dawa hii haizuii maambukizi ya magonjwa ya zinaa kama vile kisonono na kaswende, je, kukubalika kwa matumizi ya dawa hii duniani kunamaanisha ongezeko la magonjwa ya zinaa.

Friday, 3 July 2015

Chenge kubanwa Escrow kabla ya Oktoba 25.

Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge.
Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma limeeleza kuwa Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge, atahojiwa kuhusiana na kuhusika kwake katika sakata la fedha za akaunti iliyokuwa Benki Kuu (BoT) ya Tegeta Escrow kabla ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
 
Hatua hiyo ya Baraza inatarajiwa kuchukuliwa ikiwa ni siku chache tu baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutupilia mbali zuio lake la Chenge la kutaka asihojiwe na baraza hilo kutokana na gawiwo la Sh. bilioni 1.6 kutoka akaunti hiyo ya Tegeta Escrow.
 
Taarifa za uhakika ambazo NIPASHE imezipata kutoka kwenye Baraza la Maadili zinasema kuwa kabla ya uchaguzi mkuu, Chenge na wenzake watatu ambao walikataa kuhojiwa na baraza hilo kuhusiana na mgawo wa Escrow sasa watahojiwa.
 
“Tume ilikuwa imepanga kuzungumza na waandishi wa habari leo (juzi), kuzungumzia suala hilo la kuhojiwa Chenge na wenzake waliokimbilia mahakamani, lakini imeshindikana kwa sababu baadhi ya maofisa wamesafiri kikazi,” alisema ofisa mmoja wa Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
 
Aliongeza: “Siwezi kusema ni lini atahojiwa (Chenge). Lakini taarifa itatolewa kwenye vyombo vya habari, kazi hii naamini itafanyika mapema hata kabla ya uchaguzi mkuu.”
 
Baadhi ya vigogo waliokataa kuhojiwa kutokana na kuwapo kwa zuio la mahakama ni aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), Philipo Saliboko na Kamishna Upelelezi wa Kodi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Lucy Appollo. Inaelezwa kuwa Saliboko alipata mgawo wa Sh. milioni 40.4 na Appollo aligawiwa Sh. milioni 80.8.
 
Watuhumiwa waliohojiwa na kiasi walichodaiwa kupata kwenye mabano ni Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Profesa Anna Tibaijuka (Sh. bilioni 1.6); Mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja (Sh. milioni 40.4); aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Dk. Enos Bukuku (Sh. milioni 161.7); majaji wawili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Profesa Eudes Ruhangisa (Sh. milioni 404.25) na Jaji Aloysius Mujulizi (Sh. milioni 40.4); na pia aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Emmanuel Ole Naiko (Sh. milioni 40.4.
 
Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ya mwaka 1993, kifungu cha (8), kinaeleza kuwa kati ya hatua ambazo viongozi wa umma wanaweza kuchukuliwa pale wanapobainika kukiuka sheria za utumishi wa umma ni pamoja na kuonywa, kushushwa cheo na kusimamishwa kazi.
 
Nyingine ni kufukuzwa kazi na kushauriwa kujiuzulu au kuwafikisha mahakamani baada ya kuwakuta na hatia.

Thursday, 2 July 2015

Madereva wa treni wagoma.

Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta.
Zaidi ya madereva 100 wa treni ya Reli ya Kati, wameanzisha mgomo baridi kuanzia jana wakishinikiza madai yao mbalimbali kwa uongozi wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL).
 
Hali hiyo imeelezwa kuwa inahatarisha maisha ya mamia ya abiria wanaotumia usafiri huo kutokana na dereva mwenye umri wa zaidi ya miaka 60, sasa kutumiwa kuendesha treni kwa muda mrefu.
 
Treni inayoendeshwa na mzee huyo mstaafu anayefanya kazi kwa mkataba, aliyefahamika kwa jina moja la Kisanga, iliondoka jana jijini Dar es Salaam kuelekea Mwanza na Kigoma.
 
Ilitarajiwa aendeshe treni hiyo mpaka Tabora, tofauti na utaratibu wa kawaida wa dereva mmoja kuendesha treni kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro na kupokewa na mwingine.
 
Dereva anayepokea treni Morogoro hutakiwa kuendesha hadi Dodoma na mwingine huichukua hadi Tabora ambako madereva wa kuifikisha treni Kigoma na Mwanza huingia kazini.
 
Taarifa zilielezea jinsi Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) ilivyojipanga kukabiliana na mgomo baridi huo wa madereva, kwamba ni kumuandaa Mkaguzi (Inspector) wa madereva hao, Zabron Kanuti, kupokea treni kwa Kisanga pindi itakapofika Tabora na kuifikisha Kigoma.

Lowassa: Mwenye ushahidi wa rushwa dhidi yangu ajitokeze

 Aeleze nilitoa lini, wapi, kwa nani.
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amesema amechoshwa na tuhuma za kipuuzi za kumhusisha na rushwa na sasa amewataka wote wenye ushahidi wa tuhuma hizo dhidi yake wazitoe.
 
Akizungumza na mamia ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mjini hapa jana alipokuwa akirejesha fomu ya kuomba ridhaa ya chama hicho ili awanie urais kwenye uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu, Lowassa alisema kwa muda mrefu kuna watu ambao wamekuwa wakimtuhumu kwa rushwa tuhuma ambazo alisema siyo za kweli.
 
“Ninatoa changamoto kwa yeyote mwenye ushahidi wa tuhuma hizo za kipuuzi autoe. Aeleze kwa ushahidi rushwa yoyote inayonihusu, aseme nimechukua rushwa lini, kwa nani, kwa lipi na kiasi gani,” alisema.
 
Aliongeza kuwa yeye ni muadilifu, na anaposema kuwa atasimamia vita dhidi ya rushwa atafanya hivyo kwa vitendo bila kumuonea mtu wala kumuonea haya yeyote.
 
“Ndugu wanachama wenzangu, na wananchi kwa ujumla, ni lazima sasa tufike mahali tuseme imetosha. Majungu yametosha, upotoshwaji umetosha, rushwa imetosha, na kwa pamoja tunaweza kukomesha haya. Tutayakomesha kwa kusimamia ukweli, uadilifu, uaminifu na kutenda kwa haki,” alisema Lowassa katika hotuba iliyovuta hisia kwa waliokuwa wanamsikiliza.

Basi lagonga treni, wanne wafa, kujeruhi 33.

  Miongoni mwa waliokufa ni baba na mwanawe.
Basi la Fahisan Huwei, likiwa limeharibika baada ya kugonga treni ya abiria katika kijiji cha Kibaoni wilayani Kilosa jana.
Watu wanne, akiwamo baba na mtoto wake mwenye umri wa miaka sita, wamekufa papo hapo na wengine 33 kujeruhiwa baada ya basi la Kampuni ya Fahisan Huwel,  walilokuwa wakisafiria kugonga treni la abiria mali ya Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) katika Kijiji cha Kibaoni wilayani hapa,  Mkoa wa Morogoro.
 
 Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa mkoa huo, Musa Malambo, ajali hiyo ilitokea jana saa 1.30 asubuhi, wakati basi hilo aina ya Isuzu Jouney  likitokea Kijiji cha Tindiga wilayani humo kwenda mjini Morogoro.
 
Malambo alisema basi hilo lilipofika katika eneo hilo, liligonga treni hilo lililokuwa likitokea jijini Dar es Salaam kwenda Mkoa wa Kigoma kisha kupinduka mara mbili na kusababisha vifo hivyo na majeruhi hao.
 
Alitaja chanzo cha ajali hiyo kuwa ni uzembe wa dereva wa basi hilo lenye namba T837 CTN, Bakari Salehe Nyange, Mkazi wa Kilosa, kushindwa kuchukua hadhari alipofika kwenye eneo la makutano ya reli na barabara. 
 
Aliwataja waliokufa kuwa ni Sarehe Gomba (35), Mkazi wa kijiji cha Tindiga; Mama Husna (33),  wa Mamoyo; mtoto huyo Surati Mwajili (6) na baba yake aliyefahamika kwa jina moja na Mwajili (38),  wakazi wa Pugu jijini  Dar es Salaam .