Rai hiyo ilitolewa juzi wakati wa maadhimisho ya siku ya watu wenye Ualbino wilayani Maswa baada ya wazazi, walezi na watu wenye ualbino kukutana kwa lengo la kufahamiana na kufahamu haki yao ya kikatiba ya kuishi kwa mujibu wa haki za binadamu.
Katika mkutano wa pamoja jamii ya watu wa Maswa ilimwomba Rais Kikwete kuhakikisha anaweka saini hukumu zilizowatia hatiani wauaji wa walemavu hao ili kulinda heshima ya taifa la Tanzania lenye sifa ya kuheshimu na kulinda haki za binadamu ikiwamo ile ya kuishi.
Mkutano huo ulijumuisha wazazi, walezi na watu wenye ulemavu wa ngozi wakiwamo wanafunzi wa Dekapol na watendaji wa kata.
Awali mgeni rasmi katika mkutano huo ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa, Trasias Kagenzi, alilaani mauaji ya albino kwa kuhusisha na imani potofu za kishirikina kwamba kuwa na kiungo cha albino ni kupata utajiri au madaraka kwa urahisi jambo ambalo alisema ni ujinga.
Katika hatua nyingine Mkuu wa wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu, Ponsiano Nyami, alimwaga machozi mbele ya umati wa wananchi wa Wilaya hiyo kutokana na ukatili wakinyama wanaofanyiwa walemavu hao.
Kiongozi huyo alifikia hatua hiyo baada ya kwaya ya AIC (T) Bariadi,kuimba wimbo aliokuwa wa huzuni ukielezea ukatili wanaofanyiwa walemavu wa ngozi nchini, ambapo aliamua kujiunga na wanakwaya hao kuimba wimbo huo.
“Mwenyezi Mungu alitwambia tupendane…lakini alituachia upendo na amani, kwa nini tugeukane…kwanini tunakosa roho ya utu?” alihoji.
Awali, akisoma taarifa ya Mkoa, Ofisa Ustawi wa Jamii, Getruda Kulinda, alisema kuwa Mkoa wa Simiyu una jumla ya watu wenye ulemavu wa ngozi 341 na 100 kati ya hao ambao ni watoto wadogo wamepelekwa katika kituo cha Buangija mkoani Shinyanga baada ya kubainika kuishi sehemu hatarishi.
Mwenyekiti wa Chama cha Albino Mkoni hapa, Zakayo Malulu, aliiomba serikali kuwapatia matibabu bure watu wenye ualbino na viwanja bure katika sehemu zenye watu ili kuishi katika sehemu salama.
Malulu alisema kuwa serikali inapaswa kuwasaka vinara wa mauaji ya albino na kuwafikisha katika vyombo vya sheria na wanapopatikana na hatia wepewe adhabu kali.
No comments:
Post a Comment