Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu za kuomba kugombea kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia CCM, Dodoma juzi. Picha ya Maktaba
Mitandao ya kijamii ilijaa mijadala inayohusu kuingia kwake katika kinyang’anyiro hicho, huku baadhi ya wapambe wa wagombea wakieleza wazi kukatishwa tamaa na mgombea huyo ambaye wasifu wake unaonyesha ana sifa za ziada zaidi ya baadhi ya wagombea.
Dar es Salaam. Hatua ya Jaji Mkuu wa zamani wa Tanzania, Augustino Ramadhani kujitosa kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa na CCM kuwania urais imewavuruga wagombea wenzake wa urais na kuibua mjadala mzito katika maeneo mbalimbali nchini.
Mitandao ya kijamii ilijaa mijadala inayohusu kuingia kwake katika kinyang’anyiro hicho, huku baadhi ya wapambe wa wagombea wakieleza wazi kukatishwa tamaa na mgombea huyo ambaye wasifu wake unaonyesha ana sifa za ziada zaidi ya baadhi ya wagombea.
Miongoni mwa hoja zilizoibuliwa ni sifa ambazo CCM huzitumia bila kuzitaja, hasa kile kinachoitwa zamu kati ya Bara na Zanzibar na nyinginezo, ikielezwa kuwa akihitajika mgombea kutoka Zanzibar kumrithi Rais Jakaya Kikwete, Jaji Ramadhani anaonekana kufaa zaidi.
Katika mijadala hiyo, wapo waliohusisha hukumu alizowahi kuzitoa akiwa Jaji na baadaye Jaji Mkuu kwamba zililenga kukibeba chama hicho tawala kwa sababu anaonekana alikuwa na mapenzi nacho siku nyingi lakini wengine walieleza kuwa hawaoni tatizo kwa jaji huyo ambaye ni Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu.
Jaji Ramadhani ajibu hoja
Wakati maoni ya wananchi yakitofautiana juu ya hatua ya Brigedia Jenerali huyo mstaafu kuchukua fomu, mwenyewe aliliambia gazeti hili jana kwamba kwa sasa si jaji tena, hivyo ana haki ya kugombea urais na hakuna kanuni wala sheria inayomzuia.
Alitoa ufafanuzi huo baada ya kuulizwa swali kuhusu Ibara ya 113A ya Katiba ya Tanzania inayotajwa kumzuia, ikisema; “Itakuwa ni marufuku kwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji wa Mahakama Kuu, Hakimu wa ngazi yoyote kujiunga na chama chochote cha siasa, isipokuwa tu kwamba atakuwa na haki ya kupiga kura iliyotajwa katika ibara ya 5 ya Katiba.”
“Ukisoma Ibara hiyo inasema kama mhusika ni jaji. Mimi huko nimeshaondoka sasa nitashindwa kugombea kwa lipi? Wacha watu waibue mambo tu, lakini hata ukisoma Katiba utaona mwenyewe wao wanazungumzia past tense (wakati uliopita), sasa tunazungumzia present tense (wakati uliopo),” alisema.
Kuhusu mapenzi kwa CCM yanayoweza kuathiri utendaji, Jaji Ramadhani alihoji, “Hukumu gani niliipendelea? Hakuna kitu kama hicho. Kuanzia 1961 tulivyopata uhuru, majaji hawakuwa kwenye chama? Sasa kuna ajabu gani mimi kuwa katika chama maana kipindi hicho kulikuwa na chama kimoja tu, watu wote walikuwa katika chama si majaji tu.
“Zamani (wakati wa chama kimoja), ulikuwa huwezi kupata kazi ya aina yoyote kama wewe si mwanachama. Leo ajabu ni mimi tu. Hata wanahabari ilikuwa lazima wawe wanachama.”
Jaji Ramadhani ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, juzi mchana alichukua fomu kuwania nafasi hiyo ya kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano huku akisema; chema chajiuza, kibaya chajitembeza.
Katika maelezo yake alisema alikuwa mwanachama wa Umoja wa Vijana wa Tanu tangu Agosti, 1969 wakati huo akiwa mwanafunzi wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Alisema alipotuma maombi ya kujiunga na jeshi alitakiwa kuwa mwanachama wa Tanu ndipo ajiunge na jeshi na baada ya kufanikiwa kupata kadi ya Tanu aliendelea kuwa mwanachama wa CCM hadi mwaka 1992.
Alisema wakati mfumo wa vyama vingi vya siasa ulipoanza na Katiba kukataza majaji kuwa wanachama wa vyama vya siasa, alijiondoa CCM na alirejea alipostaafu ujaji mwaka 2011.
Wanasheria wampinga
Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa Chadema na mwanasheria nguli, Profesa Abdallah Safari alisema: “Anajipa moyo tu. Nchi zilizopo katika Jumuiya ya Madola, ikiwamo Tanzania, zinazuia majaji kujiingiza katika shughuli za siasa, japo wanatakiwa kufanya shughuli nyingine, ikiwamo kufundisha.
“Haki ili itendeke lazima ionekane. Inakuwaje Jaji anakaa mahakamani na baadaye kuamua kujitosa katika siasa. Akifanya hivyo inatafsiriwa kwamba akiwa jaji alikuwa akikilinda chama alichopo sasa.”
Profesa Safari alitolea mfano hukumu ya Jaji Ramadhani na wenzake sita katika kesi iliyofunguliwa na Mchungaji Christopher Mtikila ya kutaka Mahakama itambue mgombea binafsi na kusisitiza kuwa ilipingwa na wananchi, akiwamo Jaji Mkuu aliyemtangulia, Barnabas Samatta.
“Jaji Samatta aliiponda hukumu ile na kufanya Jaji Ramadhani na wenzake waonekane hawakufanya kitu. Watu walihoji iweje majaji wote saba wawe na mtazamo wa pamoja labda walikuwa wakiilinda CCM,” alisema Profesa Safari na kusisitiza kuwa uamuzi wake wa sasa utawashangaza majaji wa nchi za Jumuiya ya Madola.
Mhadhiri wa Shule Kuu ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Jesse James alisema: “Uamuzi wake unaleta utata. Hakuna sheria inayombana ila inaonekana kama aliendelea kubaki na kadi ya CCM au mapenzi na chama hicho kipindi chote cha ujaji wake.” Alisema kwa sasa Jaji Ramadhani yupo Mahakama ya Afrika na jambo hilo halileti picha nzuri kwa demokrasia nchini. “Tunaonekana hatuheshimu misingi ya sheria. Hii inaweza kuleta picha kwamba Serikali inatumia watendaji wake kwa masilahi ya chama.”
Jesse alitolea mfano jinsi Rasimu ya Katiba ya iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilivyopendekeza muda wa miaka mitano kwa watumishi wa Serikali kujiingiza katika siasa lakini kipengele hicho kikaondolewa licha ya kuwa na maana kubwa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Bashiru Ali alisema hakuna tatizo kwa Jaji Ramadhani kugombea urais, akitolea mfano Jaji Mark Bomani kuwa aliwahi kujitosa kuwania urais wakati amewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
“Kwa sasa Jaji Ramadhani si jaji tena, hivyo ana haki zote za kugombea urais. Kama angekuwa jaji, polisi au mwanajeshi angejiuzulu na kuingia katika siasa lakini kwa sasa hayupo tena huko,” alisema Bashiru.
Mtaalamu wa Lugha ya Kiswahili, Dk Aldin Mutembei alisema, “Katiba inamruhusu kugombea ni haki yake.Katiba ya CCM
Kwa mujibu wa Katiba ya CCM Ibara ya 7, raia yeyote wa Tanzania mwenye umri usiopungua miaka 18, anaweza kuwa mwanachama wa chama hicho iwapo anakubali imani, malengo na madhumuni yake.
No comments:
Post a Comment