Thursday, 25 June 2015

Muswada wa Habari usipelekwe bungeni – CCM.

Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeungana na wadau wa habari kwa kuitaka serikali kukubali kuondoa Muswada wa Habari wa mwaka 2015 bungeni ili kuurudisha kwa wadau ili uweze kujadiliwa  upya.
 
Katibu wa Itikadi na Uenezi,  Nape Nnauye (pichani), alitoa kauli hiyo juzi wakati akiwahutubiwa wananchi wa jimbo la Misungwi, mkoani Mwanza, ikiwa ni sehemu ya ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, katika mikoa ya kanda ya ziwa.
 
Nape alisema si vyema serikali kulazimisha muswada huo kujadiliwa bungeni kabla ya wadau wa habari hawajaridhika nao, kwani lengo ni kusaidia serikali na wadau wa habari na si vinginevyo.
 
Alisema  kumekuwa na mjadala mrefu kuhusu muswada huo wa habari, hali ambayo imesababisha kuwa na msuguano mkubwa kati ya Serikali na wadau wa habari nchini na hiyo ni  kutokana na vifungu vilivyopo ndani yake ambavyo vinaikosesha haki ya kupata habari tasnia hiyo.
 
Nape alisema kutokana na hali hiyo, kuna haja ya serikali kuwasikiliza wadau wa habari kwa sababu kama sheria zinatungwa na serikali huku wadau wakizilalamikia litakuwa siyo jambo jema.
 
 “Kuna vipengele ambavyo si sawa kwa mfano, mwanahabari anataka taarifa kutoka serikali atume maombi ndani ya mwezi ndipo yajibiwe na pia mtoa majibu ana hiari hiyo habari itoke au isitolewe, sasa ina maana gani kwa jamii na tasnia kwa ujumla kama taarifa itatoka ndani ya mwezi hakuna habari hapo,” alisema Nape.
 
Aliongeza kuwa kama ikitokea wadau wameikataa sheria hiyo, lakini serikali ikalazimisha ni wazi kuwa sheria hiyo utekelezaji wake utakuwa mgumu.
 
Mambo yanayolalamikiwa na wadau katika muswada ni pamoja na vifungo ambavyo vinambana mwandishi kutoa habari hadi pale aliyetoa habari atakapomtaka kufanya hivyo.
 
Pia sheria hiyo inamtaka mwandishi wa habari akienda kuchukua habari katika ofisi ya Serikali  apeleke maombi ndani ya siku 30 na hata akifanikiwa kupata habari hiyo, hawezi kuitoa hadi aruhusiwe na kama ataitoa bila kibali anaweza kufungwa kifungo cha miaka mitano jela.
 
Muswada wa Sheria ya Kupata Habari wa Mwaka 2015 unatarajia kuwasilishwa katika Bunge la Bajeti linaloendelea mjini Dodoma.  

No comments:

Post a Comment