Thursday, 25 June 2015

Akamatwa uwanja wa ndege Dar na kobe 173


Kaimu Mkurugenzi wa Uwanja wa JNIA, Clemence Jingu alisema abiria huyo mwenye hati ya kusafiria yenye namba 003870237, alikamatwa usiku wa kuamkia jana akijitayarisha kupanda ndege ya Emirates iliyokuwa ikielekea Kuwait kupitia Dubai.

Michuano ya kufuzu katika dimba la CHAN yaanza

Michuano ya kufuzu ya dimba la Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ligi za nyumbani - CHAN iimeanza na baadhi ya matokeo ya michuano hiyo yamesababisha makocha kupigwa kalamu.
Tanzania imemtimua kocha Mholanzi Mart Nooij, Malawi ikampiga teke Young Chimodzi, nayo Msumbiji ikamwambia kwaheri Joao Chisano.
Hii ni baada ya timu hizo zote zilipoteza mechi zao kza mwishoni mwa wiki. Chimodzi alipoteza kazi baada ya Malawi kushindwa mbili moja nyumbani dhidi ya Zimbabwe, wakati Chisano akifungasha virago baada ya Msumbiji kurambishwa moja bila na Rwanda.
Malawi na Msumbiji kisha zikachukua uamuzi wa haraka kuwapa majukumu ya uongozi wa muda wachezaji wa zamani wa timu za taifa Ernest Mtawali na Helder ‚ Mano Mano‘ Muianga.
Shirikisho la kandanda la Tanzania TFF limesema mrithi wa Nooij mwenye umri wa miaka 61, atatangazwa karibuni. Katika matokeo mengine Ethiopia iliishinda Kenya mbili bila wakati Zimbabwe ikipata matokeo sawa na hayo dhidi ya Visiwa vya Comoro.
Djibouti ilitoka sare ya goli moja kwa moja na wageni Burundi wakati Lesotho na Botswana zikitoka sare tasa katika mchuano mwingine. Mechi za marudiano zitachezwa wikendi ijayo huku nyingine zikichezwa wikendi ya kwanza ya mwezi wa Julai.

Muswada wa Habari usipelekwe bungeni – CCM.

Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye.
Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeungana na wadau wa habari kwa kuitaka serikali kukubali kuondoa Muswada wa Habari wa mwaka 2015 bungeni ili kuurudisha kwa wadau ili uweze kujadiliwa  upya.
 
Katibu wa Itikadi na Uenezi,  Nape Nnauye (pichani), alitoa kauli hiyo juzi wakati akiwahutubiwa wananchi wa jimbo la Misungwi, mkoani Mwanza, ikiwa ni sehemu ya ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, katika mikoa ya kanda ya ziwa.
 
Nape alisema si vyema serikali kulazimisha muswada huo kujadiliwa bungeni kabla ya wadau wa habari hawajaridhika nao, kwani lengo ni kusaidia serikali na wadau wa habari na si vinginevyo.
 
Alisema  kumekuwa na mjadala mrefu kuhusu muswada huo wa habari, hali ambayo imesababisha kuwa na msuguano mkubwa kati ya Serikali na wadau wa habari nchini na hiyo ni  kutokana na vifungu vilivyopo ndani yake ambavyo vinaikosesha haki ya kupata habari tasnia hiyo.
 
Nape alisema kutokana na hali hiyo, kuna haja ya serikali kuwasikiliza wadau wa habari kwa sababu kama sheria zinatungwa na serikali huku wadau wakizilalamikia litakuwa siyo jambo jema.
 
 “Kuna vipengele ambavyo si sawa kwa mfano, mwanahabari anataka taarifa kutoka serikali atume maombi ndani ya mwezi ndipo yajibiwe na pia mtoa majibu ana hiari hiyo habari itoke au isitolewe, sasa ina maana gani kwa jamii na tasnia kwa ujumla kama taarifa itatoka ndani ya mwezi hakuna habari hapo,” alisema Nape.
 
Aliongeza kuwa kama ikitokea wadau wameikataa sheria hiyo, lakini serikali ikalazimisha ni wazi kuwa sheria hiyo utekelezaji wake utakuwa mgumu.
 
Mambo yanayolalamikiwa na wadau katika muswada ni pamoja na vifungo ambavyo vinambana mwandishi kutoa habari hadi pale aliyetoa habari atakapomtaka kufanya hivyo.
 
Pia sheria hiyo inamtaka mwandishi wa habari akienda kuchukua habari katika ofisi ya Serikali  apeleke maombi ndani ya siku 30 na hata akifanikiwa kupata habari hiyo, hawezi kuitoa hadi aruhusiwe na kama ataitoa bila kibali anaweza kufungwa kifungo cha miaka mitano jela.
 
Muswada wa Sheria ya Kupata Habari wa Mwaka 2015 unatarajia kuwasilishwa katika Bunge la Bajeti linaloendelea mjini Dodoma.  

Saturday, 20 June 2015

Baraza la Madiwani Tabora laridhia kukamwatwa Elibariki Kingu



BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Igunga,Mkoani Tabora limeridhia agizo lililotolewa na Mkuu wa kitengo cha upelelezi wa makosa ya jinai Mkoa wa Tabora la kumkamata aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Igunga,Elibariki Kingu anayetuhumiwa kutafuna shilingi milioni 95 zilizotolewa na Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo kwa vijana mwaka 2013.

Friday, 19 June 2015

Jaji Ramadhani awavuruga wagombea urais CCM

Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu za kuomba kugombea kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia CCM, Dodoma juzi. Picha ya Maktaba 
Mitandao ya kijamii ilijaa mijadala inayohusu kuingia kwake katika kinyang’anyiro hicho, huku baadhi ya wapambe wa wagombea wakieleza wazi kukatishwa tamaa na mgombea huyo ambaye wasifu wake unaonyesha ana sifa za ziada zaidi ya baadhi ya wagombea.

Thursday, 18 June 2015

Ajali Arusha: Trafiki Saba, wanasurika kifo, gari la Polisi lagongwa


Ni baada ya dereva kusimamishwa akakataa, Trafiki wakapiga simu mbele, alipofika akakutwa askari wameweka kizuizi njiani akawagonga.

Taarifa zisizo rasmi watatu wamefariki hapo hapo
Askari saba wanusurika kifo baada ya gari yao kugongana na gari ya utalii mkoani Arusha

JK afurahishwa mchuano CCM

RAIS Jakaya Kikwete ameelezea kufurahishwa na wingi wa wagombea waliojitokeza kuomba ridhaa ya kuteuliwa kuwania urais wa Tanzania kwa tiketi ya CCM, akisema ni jambo zuri na ni ushahidi wa kiasi cha uhuru ambao umejengeka katika chama hicho.
Aidha, amesema pia msururu wa wagombea hao ambao sasa wamefikia 36, ni uthibitisho kuwa uongozi wa Tanzania katika miaka 10 iliyopita umekuwa wa mafanikio na kwamba kinyume cha hapo, wengi wasingependa kujihusisha nacho.
Pamoja na kufurahishwa huko, ameendelea kusisitiza kuwa, yeye binafsi hana mgombea urais anayempendelea kwa sababu wagombea wote ni wa kwake na wa chama chake, isipokuwa anayo kura moja tu ambayo ataitumia mwezi ujao wakati wa vikao mbalimbali kuamua nani awe mgombea Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu, 2015.

Mbowe ahukumiwa mwaka mmoja

Mwenyekiti wa chadema taifa Freeman mbowe
MAHAKAMA ya wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, imemtia hatiani na kumhukumu Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe kwenda jela mwaka mmoja au kulipa faini ya Sh milioni moja, kutokana na kesi iliyokuwa ikimkabili ya kumshambulia mwangalizi wa ndani wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

DK. Bilal ashauri urushaji wa matangazo ya runinga.

Makamu wa Rais Dk. Mohamed Gharib Bilal.
Makamu wa Rais Dk. Mohamed Gharib Bilal (pichani), ametoa wito kwa Taasisi za Elimu na Afya kutumia mabadiliko ya urushaji matangazo ya televisheni kwa mfumo wa digitali kwa kutoa elimu kwa njia ya runinga ili kurahisisha utoaji masomo ya Sayansi na Historia kwa vijana.
 
Wito huo aliutoa jana katika sherehe ya ukomo wa urushaji matangazo ya televisheni kwa mfumo wa analojia jijini Dar es Salaam na kuwahusisha wadau mbalimbali.
 
Dk. Bilal alisema taasisi zinazohusika zinapaswa kusimamia kwa ukamilifu maudhui yanayowafikia wananchi ili yatumike kwa maendeleo na kuhakikisha kuwa channel za televisheni hazitoi mafundisho yasiyofaa kwa vijana  na  kuathiri  Taifa  la kesho.
 
“Tuna changamoto kubwa ya kutengeneza maudhui ya ndani ili tutangaze utamaduni wetu ndani na nje ya nchi kutokana na mfumo wa sasa wa digitali kujaa maudhui mengi kutoka nje,” alisema.
 
 Aidha, alizishauri taasisi zinazohusika zikishirikiana na wadau wote kutafuta mbinu bora na kutumia fursa ya mfumo wa digitali kutengeneza maudhui yatakayotangaza nchi, utamaduni, kukuza utalii nchini na kuimarisha amani, utulivu na uzalendo.
 
Aliipongeza Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa usimamizi na maelekezo sahihi waliyoyatoa wakati wote wa kipindi cha mabadiliko hayo na kuvishukuru vituo vyote vya televisheni ambavyo vilitoa ushirikiano mzuri na kuwezesha mabadiliko hayo 

Jaji Mkuu mstaafu ajitosa urais CCM

  Ajinadi kwa sifa 6, Dk. Shein kuchukua fomu urais Z'bar leo.
Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani.
"Nilirudia uanachama wangu wa CCM mwaka 2011, baada ya kustaafu wadhifa niliokuwa nao kama Jaji Mkuu... Sina doa katika serikali au utumishi wangu; kwa kweli hakuna Mtanzania anayeweza kuninyooshea kidole kwa kupokea au kuhusika na vitendo vya rushwa. Kizuri chajiuza, kibaya chajitembeza..."
 
Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhan, ametangaza nia ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku akieleza kuwa licha ya kuwapo kwa utitiri wa wagombea urais, hakuna Mtanzania yeyote anayeweza kumnyooshea kidole akimtuhumu kupokea au kuhusika na vitendo vya rushwa.
 
Jaji Ramadhan ambaye ni kada wa 36 kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na chama chake kuwania kiti hicho, alisema hakuna mgombea anayemtisha kati ya wote waliomtangulia, kwa kuwa hakuna mwanajeshi anayeogopa.
 
Jaji Ramadhani alikuwa akizungumza na waandishi wa habari jana katika Makao Makuu ya CCM Mjini Dodoma, muda mfupi baada ya kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo.
 
“Sina doa katika serikali au utumishi wangu; kwa kweli hakuna Mtanzania anayeweza kuninyooshea kidole kwa kupokea au kuhusika na vitendo vya rushwa. Kizuri chajiuza, kibaya chajitembeza. Mimi ni mwanajeshi, nimestaafu nikiwa Brigedia Jenerali Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Sijui kama kuna mwanajeshi anayeogopa na hakuna mgombea ninayemuogopa; nikiogopa ina maana mimi si mwanajeshi,” alisema na kuongeza: 

Tuesday, 16 June 2015

Ajali ya basi, lori yaua 23, yajeruhi 31 Iringa.


Iringa.
Watu 23 wamepoteza maisha na wengine 31 wamejeruhiwa katika ajali ya basi iliyotokea juzi usiku katika eneo la Kinyanambo A wilayani Mufindi, barabara kuu ya Iringa –Mbeya.
 
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Iringa Pudenciana Protas, alisema kuwa ajali hiyo ilitokea jana  majira ya 1:45 usiku katika eneo la kinyanambo wilayani hapo.
 
Kamanda Protas alisema kuwa ajali hiyo iliyohusisha gari kampuni ya Another G Express yenye namba za usajiri T.927 CEF na gari ya kampuni ya Bravo Logistic (T) limited yenye namba za T.916 AQM lenye trela namba T.595.
 
Waliokufa na kutambuliwa mpaka sasa ni Lukas Pascal, Brasto Samila, Dickson Luvanda, Albert Silla, Rogers Mdoe, Eva Mbalinga, Hadija Mkoi, Clemence Mtati, Mohamed Kalika, Kastoli Mwakyamba, Damian Myala na Sillo Nziku.
 
Waliojeruhiwa ni Majoline Lupembe (23) mkazi wa Iringa, Veronica Simba (20) mkazi wa Tabora, Shadia Ally (24) mkazi wa Iringa, Mariam Mbise (23) mkazi wa Mafinda, Anita Makwela (24) mkazi wa Kilolo, Benita Sagala (18) mkazi wa Njombe, Bertha Mkoi (27),  Rahel Mavika (18) mkazi wa Mufindi, Selina Fulgence (23) mkazi wa Kigoma na  Maria Mwenda (17) mkazi wa Mafinga.
 
Wengine ni Ndipako Mbilinyi (23) mkazi wa Njombe, Alexander Mkakazii (28) mkazi wa Mafinga, Meshack Kibiki (44) mkazi wa Mafinga, Simon Jumbe (22) mkazi wa Singida, Jerry Lutego (36) mkazi wa Mafinga, Enock Kanyika (18) mkazi wa Mafinga, Deogratius Kayombo (21) mkazi wa Mafinga na Yusuph Lulanda  (22) mkazi wa Njonbe.
 
Wengine ni Petro Mwalongo (21) mkazi wa Njombe, Paulo Chane (21) mkazi wa Kilolo, Kenned Msemwa (28) mkazi wa Njombe, Mode Shiraz (21) mkazi wa Singida, Emmanuel Antony (21) mkazi wa Mwanza, Godfrey Kanyika (39) mkazi wa Mafinga, Boniface Bosha (20) mkazi wa Sumbawanga, Ambiana Meshack (35) mkazi wa Njombe, Martha Kanyika (30) mkazi wa Mafinga, Merina Tonga (miezi miwili), Yusuph Luhamba (34) mkazi wa Mafinga na wanaume wawili na wanawake wawili ambao hawajaweza kutambulika majina yao kutokana na hali zao kuwa mbaya.

Monday, 15 June 2015

Wamuomba JK asaini hukumu wauaji wa albino.


Rais Jakaya Kikwete.
Wazazi, walezi na watu wenye ulemavu wa ngozi (albinism), wilayani Maswa mkoani Simiyu wamemtaka rais Jakaya Kikwete kabla hajaondoka Ikulu kutia saini hukumu zote za mauaji ya albino zilizohukumiwa kwa washitakiwa kunyongwa hadi kufa.
 
Rai hiyo ilitolewa juzi wakati wa maadhimisho ya siku ya watu wenye Ualbino wilayani Maswa baada ya wazazi, walezi na watu wenye ualbino kukutana kwa lengo la kufahamiana na kufahamu haki yao ya kikatiba ya kuishi kwa mujibu wa haki za binadamu.
 
Katika mkutano wa pamoja jamii ya watu wa Maswa ilimwomba Rais Kikwete kuhakikisha anaweka saini hukumu zilizowatia hatiani wauaji wa walemavu hao ili kulinda heshima ya taifa la Tanzania lenye sifa ya kuheshimu na kulinda haki za binadamu ikiwamo ile ya kuishi.
 
Mkutano huo ulijumuisha wazazi, walezi na watu wenye ulemavu wa ngozi wakiwamo wanafunzi wa Dekapol na watendaji wa kata.
 
Awali mgeni rasmi katika mkutano huo ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Maswa, Trasias Kagenzi, alilaani mauaji ya albino kwa kuhusisha na imani potofu za kishirikina kwamba kuwa na kiungo cha albino ni kupata utajiri au madaraka kwa urahisi jambo ambalo alisema ni ujinga.
 
Katika hatua nyingine Mkuu wa wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu, Ponsiano Nyami, alimwaga machozi mbele ya umati wa wananchi wa Wilaya hiyo kutokana na ukatili wakinyama wanaofanyiwa walemavu hao.
 
Kiongozi huyo alifikia hatua hiyo baada ya kwaya ya AIC (T) Bariadi,kuimba wimbo aliokuwa wa huzuni ukielezea ukatili wanaofanyiwa walemavu wa ngozi nchini, ambapo aliamua kujiunga na wanakwaya hao kuimba wimbo huo.
 
“Mwenyezi Mungu alitwambia tupendane…lakini alituachia upendo na amani, kwa nini tugeukane…kwanini tunakosa roho ya utu?” alihoji.
 
Awali, akisoma taarifa ya Mkoa, Ofisa Ustawi wa Jamii, Getruda Kulinda, alisema kuwa Mkoa wa Simiyu una jumla ya watu wenye ulemavu wa ngozi 341 na 100 kati ya hao ambao ni watoto wadogo wamepelekwa katika kituo cha Buangija mkoani Shinyanga baada ya kubainika kuishi sehemu hatarishi.
 
Mwenyekiti wa Chama cha Albino Mkoni hapa, Zakayo Malulu, aliiomba serikali kuwapatia matibabu bure watu wenye ualbino na viwanja bure katika sehemu zenye watu ili kuishi katika sehemu salama.
 
Malulu alisema kuwa serikali inapaswa kuwasaka vinara wa mauaji ya albino na kuwafikisha katika vyombo vya sheria na wanapopatikana na hatia wepewe adhabu kali.
 

Tuesday, 9 June 2015

Umoja wa Mataifa watiwa wasiwasi na hali Burundi

Burundi imekataa matakwa ya vyama vya upinzani ya kumtaka Rais Pierre Nkurunziza kutogombea muhula wa tatu huku Umoja wa Mataifa ukionya kuwa nchi hiyo iko katika hatari ya kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyeweBurundi imekataa matakwa ya vyama vya upinzani ya kumtaka Rais Pierre Nkurunziza kutogombea muhula wa tatu huku Umoja wa Mataifa ukionya kuwa nchi hiyo iko katika hatari ya kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe


Msemaji wa serikali ya Burundi Philippe Nzobonariba amesema uamuzi wa wa Rais Nkurunziza kugombea muhula wa tatu ni jambo lisilojadilika na kupuuzilia mbali miito kutoka kwa wanasiasa wa upinzani ya kumtaka Rais huyo kuachia madaraka.
Serikali ya Burundi imesema pendekezo la tume ya uchaguzi nchini humo kuahirisha uchaguzi wa rais hadi tarehe 15 mwezi ujao itakuwa ni wa mwisho.
Hayo yanakuja wakati mkuu wa kamisheni ya kutetea haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa akionya kuwa kuongezeka kwa ghasia zinazofanywa na kundi la vijana wenye silaha walio watiifu kwa serikali ya Burundi ikiwemo mauaji, utekaji nyara na mateso kunatishia kuliyumbisha zaidi taifa hilo la Afrika Mashariki.
Uchu wa madaraka utaiweka Burundi pabaya
Zeid Ra'ad Al Hussein amesema kitu cha mwisho taifa la Burundi linahitaji baada ya kujenga amani kwa muongo mmoja uliopita ni kurejea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe kwasababu ya uchu wa watu walio wachache kutaka kusalia au kupata madaraka kwa kutumia kila namna.
Mkuu wa kamisheni ya kutetea haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein
Mkuu wa kamisheni ya kutetea haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa Zeid Ra'ad Al Hussein
Zeid ameelezea kushutushwa na madai ya kila mara kuwa wapiganaji wa kundi lijulikanlo Imbonerakure lenye mafungamano na tawi la vijana la chama tawala Burundi cha CNDD FDD wanafanya mashambulizi wakipewa maagizo na chama hicho, polisi,na mashirika ya kijasusi kwa kuwapa silaha, magari na wakati mwingine hata sare.
Umoja wa Mataifa umesema iwapo madai hayo yana ukweli wowote, basi yanaashiria kuwepo njama hatari mno za kuzidisha hali ya taharuki na uoga nchini Bunrundi na kuifanya hali ambayo tayari ni tete kuwa mbaya zaidi.
Takriban raia laki moja wa Burundi wametorokea nchi jirani wakihofia usalama wao lakini Nzobonariba amesema wengi wa waliotoroka wamefanya hivyo kwasababu ya uvumi unaosambazwa na wanasiasa wasio taka kuwepo chaguzi wakisaidiwa na raia wa kigeni na mashirika yasio ya serikali yanayotaka kuisukuma nchi hiyo kuelekea kuwa na ghasia.
Wanasiasa wanaompinga Nkurunziza wanasisitiza kuwa kugombea kwake muhula wa tatu ni kinyume na katiba ya nchi hiyo na mkataba wa amani wa Arusha uliofikiwa mwaka 2006.
Kalenda mpya ya uchaguzi yapingwa
Vyama vya upinzani vimepinga kalenda mpya ya chaguzi vikisema mazingira ya kuandaa chaguzi huru na haki hayajazingatiwa. Kiongozi wa chama kimoja cha upinzani Charles Nditije ametaka kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi kusimamia chaguzi hizo. Nditije ametaka pia wapiganaji wa kundi la Imbonerakure kupokonywa silaha.
Waandamanaji wakiandamana katika mji wa Ijenda wakipinga utawala wa Nkurunziza
Waandamanaji wakiandamana katika mji wa Ijenda wakipinga utawala wa Nkurunziza
Umoja wa Mataifa, nchi za magharibi na Umoja wa Afrika zimekuwa zikishinikiza pande zote mbili zinazozana nchini humo kuutatua mzozo huo kupitia mazungumzo lakini duru kadhaa za mazungumzo zimeshindwa kufikia suluhu.
Baadhi ya wanasiasa wa upinzani na makundi ya asasi za kiraia zimemshutumu mjumbe wa Umoja wa Mataifa anayesimamia mazungumzo hayo Said Djinnit kwa kuegemea upande mmoja madai ambayo maafisa wa Umoja wa Mataifa wameyakanusha.

Waziri Wasira azuru kaburi la hayati Karume, ashiriki dua.

Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira (wa pili kulia), akishiriki dua kwenye kaburi la Rais wa Kwanza wa Zanzibar, hayati Abeid Amani Karume mjini Zanzibar kabla ya kuanza ziara ya kutafuta wadhamini kwa ajili ya kuomba kuwania Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. PICHA: MPIGAPICHA WETU
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira, ametembelea na kushiriki dua kwenye kaburi la Rais wa Kwanza wa Zanzibar, hayati Abeid Amani Karume.
 
 Wasira aliingia visiwani Zanzibar juzi asubuhi ikiwa ni siku moja baada kuwasili kwa Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa.
 
 Wote wawili walionekana kwenye ofisi tofauti za CCM wakidhaminiwa na taarifa za uhakika zinaeleza kuwa hawakupata fursa ya kukutana.
 
 Lowassa alielekea kisiwani Pemba jana ambapo kwa upande wake, Wasira atakuwa huko leo.
 
 Alipofika Zanzibar, Wasira alikwenda Makao Makuu ya CCM, Kisiwandui na kuzungumza na Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar), Vuai Ali Vuai na kufanya dua kwenye kaburi la  Rais wa Kwanza wa Zanzibar, hayati Karume.
 
 Akiwa mkoa wa Mjini, Wasira ambaye pia ni Mbunge wa Bunda, alisema akifanikiwa kuwania Urais na kushinda, atatetea Muungano na Mapinduzi ya Zanzibar.
 
 Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini, Borafia Juma Silima, alisema hatua ya kujitokeza kwa wanachama wengi wanaoutaka Urais kupitia CCM, ni moja ya vielelezo vya kukua kwa demokrasia ndani ya chama hicho.
 
 Wilaya Mjini katika Mkoa wa Mjini palipofanyika udhamini kwa Wasira, ndipo penye Ikulu ya Rais, hospitali ya rufaa, Makao Makuu ya Polisi na hospitali ya wagonjwa wa akili.
 
 “Hiki ndicho chama chenye demokrasia pamoja na wingi wa wagombea, kila anayetaka atapita hapa ama kwa wenzetu wengine ili kudhihirisha kwamba hiki si chama cha mtu mmoja,” alisema.
 
 Aliongeza: “Naamini hiki kingine ni cha ufalme, mpaka aliyepo afe ndiyo arithi mwingine, sasa demokrasia imetanuka, wenye nia waje mjini hapa kudhaminiwa.” 
 
 Kwa upande wake, Wasira alisema Zanzibar inahitaji maendeleo, ustawi wa jamii na zaidi ya yote kulinda Muungano na Mapinduzi ya Zanzibar.
 
 Alisema akifanikiwa kupitishwa na CCM na kuchaguliwa kuwa Rais, ataifanya Tanzania isiruhusu Zanzibar kurudi kwenye utumwa na wanaodhani wanaishi kwa matumaini ya kurudi kwa hali hiyo (utumwa), itakuwa ni ndoto.
 
 “Nikiwa kiongozi, nchi itakuwa katika mikono salama ambayo ufisadi si sehemu yake,” alisema.

Friday, 5 June 2015

Urais CCM: Makada 10 waingia uwanjani.

Chama Cha Mapinduzi (CCM)
  Lowassa aahidi neema watumishi wa CCM, Bilal asema atarejesha miiko ya uongozi, Magufuli: Nitasimamia Ilani ya chama, Sumaye asisitiza atakufa na walarushwa.

Makinda kuongoza mazishi ya Mwaiposa Dar, Marehemu Kamishna Malisa kuzikwa Kilimanjaro.

Spika wa Bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania, Anne Makinda.

Spika wa Bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania, Anne Makinda, ataongoza waombolezaji katika mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Ukonga, (CCM) Dar es Salaam, Eugen Mwaiposa (55).
 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Dodoma na Idara ya habari, elimu kwa umma na uhusiano wa Kimataifa-ofisi ya bunge, imeeleza kuwa Spika Makinda ataongoza mazishi ya mbunge huyo ambayo yatafanyika  Juni 6, mwaka huu. nyumbani kwake Kipunguni, Dar es Salaam baada ya watoto marehemu walioko nje ya nchi kuwasili.
 
Taarifa hiyo ilieleza kuwa mwili wa marehemu umeshawasili Dar es Salaam na kupokelewa na waombolezaji wakiongozwa na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, na kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Jeshi ya Lugalo.
 
Wakati huo huo, Mkuu wa Jeshi la Magereza mkoani Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi Mwanadamizi, Venant Kayombo,  leo anatarajiwa kuongoza mamia ya waombolezaji katika mazishi ya aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Jeshi la Magereza Tanzania Bara, Onel Malisa.
 
Mtoto wa marehemu, Emmanuel Malisa, alikuwa Kamishna kuanzia mwaka 1996 hadi 2002.
 
Marehemu alizaliwa mwaka  1944, alipata elimu ya msingi, sekondari, Chuo Kikuu.
 
Alijiunga na Jeshi la Magereza mwaka 1964 na kuhitimu mafunzo ya awali ya uaskari yaliyofanyika Chuo cha Magereza-Ukonga, Dar es Salaam kuanzia Januari –Julai mwaka huo, 1964.
 

Wednesday, 3 June 2015

Madai haya ni zaidi ya Ukristo na Uislamu


Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania , Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete. 

Huyu aliandika akitetea hoja yake kwa takwimu, hata waliomfuatia nao walimjibu kwa takwimu. Hivyo hawa wote hawawezi kuwa wapumbavu kwa wanayoyaamini.

Tuesday, 2 June 2015

Fujo zaibuka baraza la wawakilishi Zanzibar kati ya wawakilishi wa CCM na CUF.

.

Waziri mkuu mstaafu Frederick Sumaye atangaza nia yakuwania urais kupitia CCM

Waziri mkuu mstaafu wa awamu ya tatu Mheshimiwa Fredericky Sumaye ametangaza nia ya kugombea nafasi ya urasi katika kipindi cha awamu ya tano kwa kuainisha viaumbele kadhaa wa kadha ikiwemo kukuza uchumi, kupambana na rushwa, kulinda viwanda kw akuboresha kilimo pamoja na kunda chombo maalumu na mahakama ya kushughulikia ufisadi na rushwa.
Akihutubia kwenye mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar-es-Salaam, waziri mkuu msataafu mheshinmiwa Fredericky Sumaye alianza hotuba yake hiyo kwa kueleza jinsi alivyoshughulikia na matataizo ya wananchi kwa kudhibiti mfumuko wa bei na kupunguza madeni ya ndani na ya nje ya Tanzania.
 
Aidha mheshimiwa Sumaye amesema kuwa kama atapata fursa ya kuteuliwa kuwa mgombea wa nafasi ya uraisi kupitia chama cha mapinduzi CCM, amesema atahakikisha anapunguza pengo kati ya walio nacho na wasio nacho, kulinda muungano kwa kudumisha amani na utulivu nchini, sanjali na kukomesha vitendo vya rushwa na ufisadi serikalini.
 
Waziri mkuu huye ambaye anatumi kauli mbiu ya uongozi bora, komesha rushwa jenga uchumi, anakuwa mwanachama wa saba kupitia chama cha mapinduzi kutangaza nia ya kuwania kuteuliwa na chama cha mapinduzi kupeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2015.
 

Mbunge wa Ukonga, Eugene Mwaiposa afariki dunia

Name:  mwaiposa.jpg
Views: 0
Size:  39.4 KB
Mama Eugene Mwaiposa enzi za uhai wake

Mbunge wa Ukonga Eugene Mwaiposa kafariki majira ya saa nne asubuhi mjini Dodoma.

Haijafahamika vema kama alikuwa anaumwa nini, lakini taarifa za awali zinasema, Amefia Rock hotel, jirani na kituo cha mafuta cha Shabiby.


TAARIFA YA NAIBU SPIKA
Bunge la jamhuri limepata msiba wa kufiwa na mbunge wa jimbo la Ukonga, alikuwa na tatizo la shinikizo la damu kwa muda mrefu, Amefariki nyumbani kwake hapa Dodoma. Nyumbani kwa marehemu ni eneo la Chaduru opposite na jengo jipya la hoteli ya Shabiby barabara ya Dar es Salaam, Mwili umepelekwa hospitali ya mkoa wa Dodoma kwa uchunguzi zaidi.

Shughuli ya Kuaga itafanyika kesho baada ya familia yake kuwasili hapa Dodoma. Tutatumia mtandao wa simu kuwajulisha taarifa zaidi, kwa jinsi hio natumia kanuni ya 152 kuahirisha bunge hadi keshokutwa Alhamis