Ndugu Wanajamii!, 
Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa uwingi wa Rehema zake na Kibali alichotupatia kuingia mwaka 2015. Hapana shaka Hakuna kati yetu anayeweza kujisifu kwa kiburi kwamba amejitahidi kwa kadri ya uwezo wake mpaka amefanikiwa kuumaliza mwaka 2014 kwa salama na kuingia 2015. Hii ni rehema yake Mungu pekee na hivyo hatuna budi kumrudishia sifa na shukrani. 
Najua pamoja na rehema na kibali tulichokipata kuingia mwaka huu, ni dhahiri pia tumetukiwa na mambo kadha wa kadha. Kuna waliopata ajali, kuna waliyosumbuliwa na maradhi mbalimbali, kuna waliopoteza Ndugu, jamaa na marafiki, kuna walioyumba kiuchumi ama kuporomoka kabisa. Hayo yote ni majaribu mbalimbali katika maisha lakini kwa kudra zake Mwenyezi pamoja na hayo yote hatimaye umefanikiwa kuvuka. Ni jambo la kumshukuru Mungu sana. Majaribu ni mtaji wa kuongeza imani, hivyo usinung`unike sana bali simama imara ili ulishinde jaribu lako. Tafakari kwa kina na kisha fanya maamuzi ya kumrudia Mungu wako kwa kumaanisha. 
Wapo ambao mambo yao hayakuwa na mushkeli hata kidogo katika mwaka wote tulioumaliza. Kila kitu kwao kilikwenda murua. Ninawasihi wasijenge kiburi na kujisahau kwamba walikuwa ni wajanja sana hata wakaweza kupita kila walipohitaji bila shida. Ninawasihi waamini kwamba haikuwa kwa ujanja, akili wala uwezo wao bali neema ya Mungu iliwashukia. 
Kwa ujumla ninawasihi Wanajamii wote kutafakari kwa kina na kwa moyo mnyeyekevu ukuu wa Mungu. Tuyatende yampendezayo Mungu wakati wote ili pamoja na kufanikiwa kwetu tujenge Taifa la wacha Mungu ama jamii inayoendesha shughuli zake zote huku ikitambua fika kwamba Mungu ndiye Mkuu na ndiye muweza wa yote duniani na mbinguni. 
Pili; Jamii yetu kwa sasa inanyemelewa ama tayari inashambuliwa na maadui wakubwa sana ambao pasipo kuwa makini na kuomba Mungu atupe Hekima, hakika tutayumba na kuangamia kabisa. Tutaandika historia mbaya kuliko zote zilizowahi kutokea katika uso wa dunia. Tutaweka rekodi hasi miongoni mwa Mataifa ya dunia hii kinyume kabisa ya historia tuliyonayo sasa ambayo kwa zaidi ya miaka hamsini (50) tangu uhuru imeshikilia rekodi ya kuwa chanya katika uso wa dunia na hivyo kuwa nchi ya kupigiwa mfano. 
Tunasumbuliwa na Ubinafsi, Unafiki, Uongo na Uzandiki katika Nyanja zote za kiuchumi, kisiasa na hata kiutamaduni. Hali hii imepelekea kuwepo na vitendo vya RUSHWA ambayo imeendelea kukomaa zaidi kwa takribani kipindi cha miongo mitatu na sasa kutishia kuwa Jabali ambalo kila mtu analiogopa kuliangusha. Imepelekea kuwapo na hali ya UDINI na UKABILA, moja kati ya maradhi hatari sana kuyaugua tena ambayo hugharimu sana Taifa linapofikia katika hali ya juu zaidi ya ubaguzi wa aina hii. Imepelekea kuwapo na UKATILI na MAUAJI ya kutisha ambayo kwa akili ya kawaida mtu hawezi kuamini kinachoonekana. Imepelekea kuwapo na DHULUMA na UKOSEFU WA HAKI jambo ambalo kimsingi linahatarisha AMANI ya nchi. Imepelekea kuwapo na UFUKARA (Umasikini) wa kiwango cha juu kiasi cha kupoteza uwezo wa kutenda yaliyo ya kibinadam na badala yake kuwa na Matukio ambayo hata Msingi wake ni mgumu kufikirika. 
Labda kwa ufupi tu nitoe tafsiri yangu ya maadui hawa ili tuweze kwenda sambamba katika kile ninachozungumza:-

Ubinafsi:- ni hali ya mtu kujifikiria yeye peke yake pasipo kuwaza mtu au watu wengine. Mtu anaamua kuchimba mtaro wa kutoa maji machafu ndani ya nyumba yake lakini rahisi alichokiona ni kuyamwaga nje ya ukuta wake wa uzio pasipo kujali kwamba ile harufu mbaya ya maji hayo aliyoikataa sasa inawaendea watu wengine ambao tena kimantiki hawana hatia wala sababu ya kuipata harufu hiyo kwa kuwa hata maji yenyewe hawakuyatumia wao. Laiti kama mtu huyu angefikiria adha ya harufu mbaya ya maji machafu inavyomkera yeye ndivyo inavyowakera wengine basi asingalithubutu kufanya hicho alichokifanya kwani angejiuliza kwa swali fupi tu “hivi jirani angeyaelekeza maji haya machafu kwangu ningejisikiaje?”Ubinafsi huzaa mambo mengine kama unafiki, Uongo, uzandiki nk. 
Unafiki:- Ni hali ya mtu kujifanya ama kujidai hakerwi na kitu fulani ama hali fulani unayomfanyia au anayofanyiwa na mwingine hasa pale wanapoonana ana kwa ana. Mnafiki hathubutu kuusema ukweli wake halisi juu ya hali au jambo fulani na badala yake husengenya ama kuteta pembeni na mtu mwingine ili hali Muhusika sahihi wa suala hilo akiwa hayupo. Humuona mbaya wake ni mtu mwema sana na kumsifia kwa mbwembwe nyingi kila anapokuwa naye lakini “humponda ama kumnanga” sana pindi tu anapompa kisogo. Haya ni matunda ya ubinafsi. Alama za mnafiki ni tatu
 Kusema uongo
 Kutotumainika
 Kutotimiza ahadi
Uongo:- Ni hali ya kushuhudia jambo usilokuwa na uhakika nalo. Kusema kitu usichokijua undani wake wala chimbuko lake. Wapo watu ambao wao wakisikia tetesi za jambo fulani hulishupalia na kuliongezea “Chumvi” ili wengine waliafiki na kuliona ni jambo la kweli. Hii hutokana hasa na uvivu wa kufikiri kwa mnena uongo na hali kadhalika mpokea uongo ambaye naye huushadidia kuwa kweli. Hili ni tunda linguine la Ubinafsi. 
Uzandiki:- Ni ule uongo mkubwa uliojaa uchochezi na mambo mengine kadha wa kadha ambayo huleta adha mbaya kwa jamii. Mfano wake ni mfumo unaotumika sana na wanasiasa kwa sasa katika kuvilinda vyama vyao ama hata kuzilinda nafasi zao za kiuongozi katika kada mbalimbali. Hii ni hatari sana na pia ni zao la Ubinafsi wa hali ya juu. 
Maadui hawa wote walianza kama tetesi lakini sasa wamekuwa waziwazi kabisa na watu hawaoni haya kuyaongea ama kuyatenda mambo haya hadharani. Kuwapo na hali mbaya zaidi ya kiuchumi na hivyo kufanya ufukara (umasikini) kushamiri kwa kiwango cha hali ya juu sana. Pengo baina ya walionacho na wasionacho linadhihirika pasi na shaka wala hakuna haja ya kufanya utafiti ili kujiridhisha, ni hali iliyo bayana kabisa. 
Mazingira Halisi katika Mahospitali, Mashule, Ujenzi wa Kifisadi wa miradi mbalimbali ya maendeleo, Uharibifu wa miundo mbinu iliyokwishawekwa na serikali, mifumo ya Uendeshaji wa siasa katika vyama vyetu, mienendo ya mihimili ya kiutawala katika nchi, Mauaji ya Albino, Vikongwe, Vibaka na mauaji mengine yenye harufu za kishirikina ama kusadikiwa kuwa wivu wa kimapenzi, Ukatili wa Kijinsia, Kuongezeka kwa idadi ya watoto wa mitaani na wanaoishi katika Mazingira magumu, ongezeko la makundi ya vijana wanaoathirika na madawa ya kulevya, ukatili dhidi ya watoto, yaliyojiri katika Bunge Maalumu la Katiba na mustakabali wake kwa sasa, Mapambano yasiyokuwa na sababu ya kutokwisha ya Wakulima na Wafugaji, wimbi la ajali za barabarani zinazoendelea kugharimu maelfu ya maisha ya Ndugu, Jamaa na Marafiki, Ukiukaji wa makusudi wa maadili ya Uongozi pamoja na mambo mengine chungu mzima kamwe hatuwezi kuyatenganisha na UBINAFSI, UNAFIKI, UONGO na UZANDIKI.
Katika hotuba yake mwaka 1995 katika Mkutano Mkuu wa CCM wakati wa kuteua mgombea wa chama katika ngazi ya rais Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa hili alisema na kuwasihi wajumbe wa mkutano mkuu yafuatayo:-
“Teueni mgombea atakayekidhi matarajio ya Wananchi, acha matarajio yako wewe mpiga kura” Hapa alimaanisha wapiga kura katika mkutano mkuu wa chama utakaoteua mgombea wa urais wasiwe wabinafsi na kuteua mgombea atakayekidhi matarajio yao pekee bali kwa mapana wanapaswa kuwafikiria wenye nchi kwa mamilioni ya idadi yao kama mgombea huyo ataweza kukidhi matarajio yao katika nchi kwa ujumla. Mwalim Nyerere hapa alipinga Ubinafsi akiamini ni moja kati ya sumu mbaya sana inayoweza kuliangamiza Taifa. Ukimteua mtu kwa matarajio binafsi na kwa bahati mbaya akapita na wananchi wakamchagua kuwa kiongozi ni dhahiri Uongozi wake katika ngazi yoyote ile utaendelea kuwa wa KIBINAFSI kwa sababu alipatikana kwa UBINAFSI. 
Mwalimu Nyerere aliendelea katika hotuba yake na kusema “Watanzania kuna mambo ambayo wanataka raisi wa awamu ya tatu ayafanye, yapo mengi tu lakini mimi nitataja machache yatawatosheni. La kwanza, nitataja manne”. La kwanza; Watanzania wamechoka na Rushwa, La pili; Umasikini, La tatu; Udini na La nne; Ukabila.Mwalimu aliamini kwamba kwa wakati ule hali ya mambo haya ilikuwa mbaya zaidi nchini sijui leo Mwalimu angesemaje. Kukomaa kwa hali ya UBINAFSI, UNAFIKI, UONGO na UZANDIKI kumezidi kuyashamirisha mambo mengi aliyoyataja na hata mengine tunayoyaona leo. 
Katika haya mengi yamesemwa sana, kwa upande mmoja wapo waliowalaumu Viongozi, wapo waliowalaumu wanasiasa na vyama vyao lakini kwa upande mwingine Viongozi na wanasiasa pia walirusha lawama kwa wenye nchi (Watanzania) katika kile walichokiita uvivu na utegemezi kwa serikali yao kwamba itawafanyia kila kitu. Mimi binafsi ninachelea kusema kwamba pande zote mbili zinastahili lawama za haya yote, hata hivyo zuri zaidi na linaloleta faraja ni kwamba uwezo wa sote kubadilika kama nchi tukitaka na kuamua leo tunao isipokuwa tunakosa uthubutu kwa sababu ya Ubinafsi, Unafiki, Uongo na Uzandiki. 
Tukiwatazama maadui hao wanne tunawaona ni kama wanafanana lakini ukweli ni kwamba kila mmoja ana Uzito wake wa pekee. 
Jamii ya Wenye nchi hii, niwasihi kwamba katika mwaka huu wa 2015 wachukue hatua za kufanya tafakari za kimantiki ili waweze kusema HAPANA kubwa kwa maradhi hayo. Badala ya kuburuzwa na matakwa ya mtu yasiyojulikana na yaliyojaa Ubinafsi ni vyema tukafungua bongo zetu na kuwaaibisha maadui hao kwa mambo yafuatayo:- 
Mosi:- Kujitambua na Kutambuana, Pili:- Kujituma na Kuwajibika, Tatu:- Kuzijua Haki za raia na Sheria za nchi, Nne:-Kutovifia vyama na badala yake Tuifie Nchi. Haya mambo manne tutaendelea kuelimishana kadri Mwenyezi Mungu atakavyotujalia neema yake kupitia ukurasa huu wa “NAKUMBUSHIA TU!”. 
Mungu atusaidie katika hilo, aibariki Tanzania na Watu wake!. 
MGENI AMEINGIA 
Kwenu Wanajamii amekuja mgeni, mgeni ambaye kwa jina hatofautiani sana na mliokwishakuwapokea pengine tofauti yake ni maudhui yake anayoyaleta kwa jamii.

Hata hivyo; nimetangulia kuyanena hayo machache kama Utangulizi kwa sababu pamoja na kazi kubwa zitakazofanywa na Blogu hii ni kuelimishana katika masuala mbalimbali pamoja na kutambua fursa mbalimbali
zinazopatikana ndani ya nchi yetu ili kila mwanajamii awajibike kwa namna yake katika Ujenzi wa Taifa hili ambalo si changa tena. 
FOFAM MEDIA BLOG ni miongoni mwa mitandao mingine mingi ya kijamii ambao umedhamiria kuiletea jamii habari mbalimbali lakini kubwa zaidi ni kuhamasisha fursa zilizopo kwa elimu na mada mbalimbali zitakazowekwa katika Mtandao huu na wataalamu waliobobea au kutoka katika vyanzo vingine vya ndani na nje ya nchi.
Kwa nafasi ya pekee kabisa niwapongeze wanablog wote ambao mpaka kufikia sasa wamekwishafanya kazi kubwa sana ya kuifikia jamii kwa mambo mbalimbali yanayojiri pande zote za dunia. Ushirikiano umekuwa ni jambo la Msingi miongoni mwenu, nami pamoja na timu nzima ya FMB tuwahakikishie kwamba hatutakuwa tofauti nanyi katika ushirikiano kwa kila lenye tija na manufaa kwa Taifa hili. 
Niwaombe tu wadau wetu kwamba hii ni fursa nyingine kama zilivyokwishakutolewa na mitandao mingine kabla ya FMB, ustaarabu ni jambo litakalopewa kipaumbele zaidi ili kila mmoja wetu apate fursa iliyokusudiwa, apate habari, elimu na hatimaye aweze kuchukua fursa iliyojitokeza. Uongozi na Utawalwa wa FMB hautasita kumchukulia hatua stahiki yeyote atakayeonekana amekosa uungwana, ustaarabu na uzalendo Ikiwa ni pamoja na kumfikisha kwa mamlaka zinazohusika ili sheria ichukue mkondo wake. 
Maadui waliotajwa hapo awali kwa namna yoyote hawatakuwa rafiki wa FMB na hivyo chochote kitakachoonekana kinakwenda kinyume na dhamira halisi ya kuhabarisha, kuelimisha na kuwapa watu fursa hakitakuwa sehemu ya Mtandao wa FMB. 
Kwa ajili ya kuukaribisha mwaka mpya, tumeamua kutoa fursa ya matangazo matano ya kwanza kutufikia bure kwa mwezi wote wa Januari, 2015. Usikubali kupitwa na Ofa hii kwani fursa ipo wazi kwa kila mtu, Taasisi au kampuni bila ya kujali ukubwa wake. 
Najua imekuwa ni ndefu kidogo lakini sikuwa na budi. Niwakaribishe sana katika FOFAM MEDIA BLOG na hapana shaka mtafaidika na ujio wa Blog hii.  
Heri ya Mwaka Mpya 2015 kwa wote!!

No comments:

Post a Comment