“PANYA ROAD” NI DHAMBI ILIYOLELEWA
Wahenga walituachia urithi wa makanyo au maonyo mbalimbali kupitia misemo, nahau na hata methali ambazo kwa wakati ule ilitumika vyema katika kuhakikisha kwamba maadili kwa jamii husika yanalindwa tena si kwa gharama kubwa. Utii ulikuwa wa kiwango cha juu kwa watu wa rika na jinsi zote na hivyo jamii hizo mambo yaliwaendea murua kabisa.

Walisema; “Usipoziba ufa utajenga ukuta, Mzahamzaha hutumbua usaha, Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo, Mdharau mwiba utamchoma, Mchelea mwana hulia yeye, ukupigao ndiyo ukufunzao” na mengine kadha wa kadha kama hazina isiyokauka.

 Kwa bahati mbaya sana tumejikuta kadri miaka inavyozidi kwenda ndivyo tunavyozidi kupuuza hazina hizi huku tukiziimba kwa nadharia tu mashuleni na mitaani pasipo kuwa na mrejesho wowote wa vitendo katika maisha halisia tunayoishi kila siku. Mara nyingi tunaona kama ni misemo iliyopitwa na wakati huku tukijidanganya na maendeleo hasi yasiyo na tija kwa kizazi hiki wala kile kitakachofuata.

Katika makala yangu iliyopita ya kufungua mwaka 2015 niliwaongelea maadui wanne ambao kimsingi wanaendelea kulitafuna Taifa hili usiku na mchana mithili ya mchwa. Maadui hao ni Ubinafsi, Unafiki, Uongo na Uzandiki ambao ndiyo wanaobeba dhima kubwa ya Uchambuzi wa mwaka huu katika nyanja mbalimbali. Enzi hizo wakati tukiwa Wadogo hatukuchagua wazazi wala wazazi hawakuchagua watoto. Mheshimwa Salma Kikwete, Mke wa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Taasisi yake ya UWAMA anayo kauli mbiu yake “mtoto wa mwenzio ni wako”. Hii ni moja kati ya kauli mbiu ninazoziheshimu sana kutoka katika Taasisi binafsi ukiachia mbali ile ya Twaweza inayosema “mabadiliko ni mimi, ni wewe, ni sisi” na ile ya Haki Elimu inayosema “Tafakari, Chukua hatua”.

Nimezinukuu kauli mbiu hizi kwa maana kubwa sana. Mosi; kama tukiitekeleza kauli mbiu ya WAMA kwamba “mtoto wa mwenzio ni wako” hakika ni rahisi kurejea katika zama zile za kutochagua wazazi wala kutochagua watoto. Jamii inakubali kwa dhati kabisa kuhakikisha kwamba malezi ya mtoto ni ya jamii nzima na wala si ya familia moja. Ubinafsi katika malezi ya watoto umeendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa sana mmomonyoko wa maadili katika jamii. 

Wazazi wengi wamejifunika miavuli ya “Haki za Watoto” na “Haki za binadamu” huku wakijifanya vipofu wa tafsiri Halisi. Watoto wengi wamelelewa wakiamini kwamba wanawajibika kwa wale waliowazaa peke yake na kamwe hawawajibiki kwa wazazi wengine wowote katika jamii wanayoishi. Wanafundishwa kuwa wabinafsi Kuanzia utotoni mpaka wanakuwa watu wazima na kuwa sehemu ya tegemeo la jamii husika. Siku hizi haishangazi kuona mtoto mdogo akimsonya ama pengine kumtukana kabisa mtu wa rika sawa na baba yake ama mama yake. Anafanya hivyo akiamini kabisa kwamba kwa ubinafsi aliofundishwa hata kama mtu mzima huyo atakwenda kumshitaki kwa wazazi wake hatapata kitu zaidi ya kufukuzwa, kuzomewa na hata wakati mwingine kupigwa, hivyo kiburi kimefunika ufahamu wake na hekima imepotelea gizani. 

Siku moja nilikuwa Haydom – Mbulu Mkoani Manyara nikihangaika kupanda Basi la Hamandos kutoka hapo kuelekea Kijiji cha Dominiki Wilayani Mkalama huko Singida. Tukiwa tunaendelea kuingia ndani ya basi hilo akatokea binti mmoja anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka ishirini hadi ishirini na mitano hivi akimgombeza babu anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka kama sabini ama zaidi kwamba kwa nini amekaa kwenye kiti chake ili hali yeye ndiye aliyepewa kiti hicho. Kutokana na maneno makali sana aliyoyatoa yule binti kwa babu Yule na pia umri wa babu kutokuwa na uwezo wa kupambana na binti yule kwa maneno ya kifedhuli yule babu alisimama kisha yule binti akakaa kwenye kiti. Juhudi za abiria kwa maneno ya kawaida ya kumkanya binti yule hazikuwa na Uzito na wala hazikuzaa matunda lakini kijana mmoja ambaye bado kiumri anamzidi binti yule akaamua kusimama na kumpisha babu yule kwenye kiti chake akae. Lakini kilichotia simanzi zaidi ni pale Mama wa Binti huyo alipokuwa akicheka tu wakati mwanaye akitoa maneno mabaya kwa mtu mzima wa umri wa Babu yake. Nikajiuliza sana na kusikitikia hali ya ubinafsi ilivyoshika kasi ya ajabu katika jamii. 

Lakini hapa pia nikauona Unafiki wa Makondakta wa basi hilo na abiria kwa ujumla. Makondakta ambao kwa macho yao walishindwa kutambua umri wa yule babu na kuhakikisha hapati usumbufu, nao wakajifanya kumshangaa yule binti kwa kauli zake hata kuthubutu kuongopa kwamba siti ile ilikuwa ni ya yule babu ili hali tiketi ya binti pia ilionyesha siti hiyohiyo. Baadhi ya abiria walitetea bila kujua wanatetea nini, wengine wakijaribu kujiweka upande wa Makondakta kwa maslahi binafsi, wengine upande wa yule binti kwa kile walichoamini alikuwa na haki na wengine wakijiweka kwa Yule babu kuonyesha wanamtetea lakini wasiwe tayari kumpisha viti vyao licha ya kuwa karibu na tukio. Hii yote ilikusanya maadui wote wanne kwa pamoja.

Pili; Kwa mfano huo wa kilichojili kwenye basi nikawakumbuka TWAWEZA na kauli mbiu yao “Mabadiliko ni mimi, ni wewe, ni sisi”. Kwa kuitafakari kwa kina nikagundua makusudi halisi ya kauli mbiu hiyo ni kufanya mshikamano ambao utaweka mambo sawa kwa manufaa si ya mtu mmoja bali jamii na Taifa kwa ujumla. Nikaona Taasisi hii imechukua jukumu kubwa la kupambana na hali ya Ubinafsi uliokithiri katika jamii yetu hivi leo. 

Mara nyingi sana jamii yetu imekuwa ikizama katika bahari ya malalamiko katika kila jambo hata lile ambalo lingeweza kurekebishwa kama kila mmoja angejihesabia Wajibu na kisha haki ikafuata. Kila mtua aanze kwa kusema nimefanya nini katika kambo hili, kisha aseme umefanya nini katika jambo hili na hatimaye aseme tumefanya nini katika jambo hili. Tukiweza kuanza na mimi halafu mengine yafuate katika utekelezaji wa Wajibu tulionao katika jamii na tukaendelea kuamini ushirikishaji mzuri kwa mwingine na wengine huku tukiangalia maslahi mapana kwa jamii na Taifa mafanikio yake hayana maswali yasiyo na majibu. 

Tatu; Haki Elimu kauli mbiu yao inatuambia “Tafakari, Chukua Hatua”. Kama nilivyoeleza hapo awali maadui wetu hao hawawezi kutokomezwa pasipo tafakari za kina kama wanajamii na Taifa kwa ujumla na kisha kuchukua hatua stahiki za kukiokoa kizazi hiki na kijacho katika hali ya sintofahamu. Kauli mbiu hizi ni falsafa pana sana ambazo zikichambuliwa kwa Uzito wa hali ya juu, pekee zinaweza kutosha kulikomboa Taifa hili na majanga mbalimbali yanayoweza kuepukika. 

Kwa bahati mbaya sana machapisho ya Taasisi hizi kwa jamii wakati mwingine yamechukuliwa kwa wepesi sana na wenye dhamana na hata wananchi kwa ujumla wake. Wengine wamefurahia michoro, wengine wamefurahia malipo, wengine wamefurahi kazi wanazopewa na Taasisi zenyewe lakini hawajajikita kutathmini na kutafakari kwa kina maudhui ya kauli mbiu kama hizi kwa manufaa ya jamii na Taifa. 

Tukirejea katika misemo, nahau na methali za wahenga kama nilivyotangulia kuzitaja hapo awali japo kwa uchache tu najiuliza maswali mengi sana. Narudi nyuma kidogo mwanzoni mwa miaka ya tisini nakutana na kundi la uhalifu la KOMANDO YOSO mithili ya haya ya sasa ya Mbwa mwitu, Sisimizi, Panya Road nk ambayo pia yalihusisha vijana wa umri mdogo sana na wakati huo Mh. Agustine Lyatonga Mrema akiwa Waziri wa Mambo ya ndani. Watoto hawa watukutu waliathiri sana maeneo ya Mabibo, Manzese, Tandale, Tandika na Mbagala. Sikuyasikia makundi haya ya Watoto watukutu maeneo ya Upanga, Oysterbay, Masaki na kwingineko ambako waishio huko wanayo hadhi fulani katika nchi hii. Hata hivyo kundi hilo lilitokomezwa kabisa kwa wakati huo. 

Leo hii tunapoongelea manyanyaso ya Vikundi hivi tunayaongelea karibia maeneo yaleyale yaliyowahi kuathiriwa wakati ule na kwa jamii karibia inayofanana. Je kulikoni?? Nauona Ubinafsi Kuanzia ngazi ya familia mpaka Taifa kwa mamlaka mbalimbali za kiutendaji, Nauona Unafiki kwa ngazi hizohizo, nauona Uongo uliokithiri ama Uzandiki kwa ngazi hizohizo pia kiasi cha kuhatarisha Amani.

Watoto hawa watukutu ni wetu, tunaishi nao Majumbani ama mitaani kwetu, tunafahamiana nao mpaka na jamaa zao, wanao jamaa zao ambao ni watendaji wa ngazi mbalimbali za kimamlaka pengine pia hata katika mmoja wa mihimili mitatu (Bunge, Serikali/Dola na Mahakama) lakini tatizo linazunguka katika maadui tulionao. Ni nani atajitoa kimasomaso kumpeleka katika vyombo vya sheria mtoto wa X ambaye hakuna shaka yoyote ni muhusika wa uhalifu lakini kwa bahati mbaya mmoja wa wazazi wake anao uhusiano wa kinasaba na mdau katika mihimili na tena yule mkuu na mwenye mamlaka sehemu fulani aliwezeshwa nafasi hiyo na Marehemu mjomba ake X wakati akishikilia wadhifa mkubwa ndani ya moja kati ya mihimili. Hofu kubwa inatanda yanapokumbukwa yaliyomkuta Y ambaye alipojitoa mhanga kuhakikisha mambo hayaendelei kuharibika kwa mtoto wa X, alipotea katika mazingira ya ajabu ama alipoteza kazi ama alibambikiwa kesi mbaya na bado anasota rumande mwaka wa pili sasa. Hapo jirani yake X na Y anaishia kusema ngoja nihame huku niende sehemu nyingine shauri yao na mtoto wao. 

Mazingira ya kukithiri kwa Ubinafsi, Unafiki, Uongo na Uzandiki yanaplekea maamuzi ya “mtoto huyu si wangu watajua waliomzaa”, yanapelekea “wao ndio wanapaswa kuhakikisha mabadiliko kwani ndiyo wanaoishi huko”, yanapelekea “Hamna haja ya kumchukulia hatua mtoto wa mwingine”, yanapelekea kutoa taarifa za kumficha mhalifu kwa vyombo vya usalama, kudhani hakuna shida ili hali hali si shwari, kutafuta urafiki wa mashaka, kuvunjika kwa amani katika maeneo fulani na mambo chungu mzima. 

Tunao “Panya Road” wa aina nyingi tuliowazalisha na kuwalea kwa Ubinafsi wetu na kupelekea mambo mengi kuwa shaghalabaghala, maadili kumomonyoka na mambo kadha wa kadha. Wapo panya road katika kila sekta ijapokuwa majina yanaweza yakatofautiana. Tumevamiwa na panya road Kisiasa, Kiuchumi na Kiutamaduni ambao vita yake ni zaidi ya kuwa na vijana wa Kamanda Kova au IGP Mangu mitaani. Umma wa Watanzania unatakiwa uazimie kwa kauli moja kuchukua hatua ya kutokomeza Panya road katika nyanja zote ili kulinusuru Taifa hili. Mamlaka zinazohusika hazina budi kuhakikisha hazimuangalii nyani usoni inapobidi kumuua, nikimaanisha ni vyema sheria ikachukua mkondo wake bila kujali mahusiano ya aina yoyote baina ya mhalifu na wale walioshika mipini. 

Nakumbushia tu, makundi ya ugaidi ya Boko Haramu, Al Shabaab, Al Qaeda na mengineyo yasiyosikika duniani yamekuwa ni matendo ya kukithiri kwa Ubinafsi, Unafiki, Uongo na Uzandiki. Kwa mujibu wa Mtandao wa Wikipedia Boko Haram ilikuwa tayari imeua watu zaidi ya elfu tano (5,000) kati ya Julai 2009 mpaka Juni 2014, kundi hili lilianzishwa mwaka 2002. Al Shabaab iliyoanzishwa mwaka 2006 kama tawi la Al Qaeda mpaka sasa imeleta madhara makubwa Somali na hata nje ya Somali na Al Qaeda iliyoanzishwa 1988 hakuna asiyejua kilichotokea na kinachoendelea bila kuhusisha itikadi za kiimani.

Kwa Tanzania pia tumekwishaanza kuonja mambo ya vitendo na matunda ya kukithiri kwa ubinafsi, unafiki, uongo na uzandiki kama ilivyotokea Zanzibar, Arusha, Iringa na hata Dar es Salaam. Tunahitaji muda mfupi sana wa kujitathmini, kutafakari kama tupo salama bado kisha tuchukue hatua kwani mchelea mwana hulia yeye. 

Tufanye mambo yetu lakini wakati mwingine tukae karibu sana na misemo, nahau na methali za wahenga. Kwanini tuingie gharama ya ukuta kama inawezekana kuziba ufa na nyumba ikawa nzuri?. Kama wanavyofanya Panya Road sivyo kwanini hatuwafanyi watoto hawa wakue kadri tunavyopenda wawe wakikua?. Kwa kuyajua madhara ya mwiba hatupaswi kuudharau hata ukiwa mdogo maana kadri unavyokua utakuja kuleta madhara makubwa. Hatuhitaji kulia sisi hapo baadaye kwa kuwa tuliyakenulia meno kila waliyofanya watoto wetu ili kukidhi haja za muda mfupi kwa madhara endelevu. Chondechonde; tujifunze sasa kwa litupigalo kama hatukufanya hivyo pale awali. Wizara ya mambo ya ndani bado pia inaweza kumshirikisha Mh. Mrema ama wakuu wa Polisi waliotangulia kujua mbinu gani mbadala zilitumika kupambana na Komando Yoso ambalo ni kama haya ya sasa na kuhakikisha kwamba hayajirudii tena. 

Serikali za mitaa kwa nafasi zao wakishirikiana na wajumbe wa nyumba kumi bila kujali itikadi zao za kisiasa wahakikishe kwamba elimu ya kutosha inatolewa kwa vijana juu ya Wajibu wao kwa Taifa na Jamii inayowazunguka kwa ujumla. Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ziwawezeshe watendaji wake katika ngazi zote kuhakikisha kwamba raslimali watu na hasa hii ya vijana haichezewi hovyo bali inapewa fursa za kutosha ili kushiriki Ujenzi wa Taifa. 

Kila mtu katika nafasi yake avue joho la Ubinafsi na Kofia ya Unafiki, atupe saa ya Uongo na Pete ya Uzandiki badala yake vazi moja tu la Uzalendo kwa Taifa litoshe kuifanya nchi hii ipendeze. 

"Mtoto wa mwenzio ni wako", "Mabadiliko ni mimi -ni wewe - ni sisi", "Tafakari – Chukua hatua". Ahsante, WAMA, TWAWEZA na HAKI ELIMU kwa kauli mbiu zenu zenye tija kwa Taifa tukizitumia vyema tutavuka salama.


Soma zilizopita

No comments:

Post a Comment