Dodoma. Wabunge wameitaka Serikali kutofanya
haraka kuanzisha kitengo cha deni la Taifa hadi hapo kutakapokuwa na
wataalamu wenye weledi wa kutosha.
Walisema hayo juzi katika semina ya Kamati ya
Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara iliyoandaliwa na Taasisi ya
Tanzania Coalition on Debt Development (TCDD).
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dutsun Kitandula
alisema deni hilo limesemwa na wananchi kwa muda mrefu na kwamba
wabunge nao wana wajibu wa kulijadili.
“Tusifanye haraka, ni lazima tujifunze na kujipa muda wa kupata wataalamu,” alisema Kitandula.
Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Cecilia Pareso
alisema Serikali inapotaka kukopa, lazima ieleze ni kiasi gani inakopa,
italipa lini na riba ni kiasi gani.
“Kwa sababu Taifa linapokopa, kila mtu anadaiwa kama siyo leo, basi ni kizazi kijacho,” alisema Pareso.
Mbunge wa Nkasi (CCM), Ally Keissy alisema deni
hilo limekuwa kubwa kwa sababu Serikali huwapa dhamana wafanyabiashara
waliofilisika.
“Fedha zenyewe hazikusaidia wananchi wala kujenga barabara, Taifa halikunufaika pia,” alisema Keissy.
Mkurugenzi Mtendaji wa TCDD, Heribon Mwakagenda alisema deni la Taifa limefikia Sh30 trilioni.
Alisema: “Ni bora wakati mnatunga sheria kuwe na udhibiti zaidi.
“Serikali ikiomba kibali inapotaka kukopa, lakini kuwe na kikomo ambacho nchi haiwezi kukopa tena,” alisema.
No comments:
Post a Comment