Lowassa amepanga kuchukua fomu kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) akitokea Makao Makuu ya Chama cha Wananchi (CUF), yaliyopo Buguruni jijini Dar es Salaam na baadaye msafara huo utaishia Ofisi Kuu za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Kinondoni.
Kote huko, Lowassa atasindikizwa na viongozi, wanachama na wafuasi wa vyama hivyo, huku taarifa nyingine zikieleza kutakuwapo na wafuasi wake waliokuwa wakimuunga mkono alipokuwa CCM.
Ni safari inayotarajia kutimiza takriban kilomita 10 kwa umati huo kutembea wakimsindikiza Lowassa kutoka Buguruni hadi Posta (kilomita sita) na kuendelea hadi Kinondoni (kilomita 4). Ukawa unaundwa na vyama vinne ambavyo ni Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD).
Kaimu Katibu Mkuu Mwenza wa Ukawa, Salum Mwalimu, alisema jana kuwa Lowassa atafuatana na mgombea mwenza, Duni Haji.
Akizungumza kwenye ofisi za Makao Makuu ya NCCR-Mageuzi jijini Dar es Salaam, Mwalimu alisema Lowassa atakwenda Nec akitokea ofisi za Cuf zilizopo Buguruni saa 3:00 asubuhi.
Alisema mara baada ya kutoka Nec, msafara huo utaelekea Chadema ambapo huko wataendeleza shamrashamra kwa wagombea wao.
Mwalimu alisema ratiba ya wagombea hao kutafuta wadhamini kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi itaanza Ijumaa ijayo.
Ratiba ya Ukawa inaonyesha kuwa Alhamisi ijayo, Lowassa atashiriki mazishi ya aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la CCM, marehemu Peter Kisumo huko Usangi mkoani Kilimanjaro.
No comments:
Post a Comment