
VITA kubwa kwenye Ligi Kuu ya England sasa imehamia kwenye tuzo ya
mchezaji bora wa mwaka wa ligi hiyo ambapo wanaume wawili wanapambana
vikali.
Vita hiyo ipo kati ya kiungo wa Manchester City, Kevin De Bruyne, na
mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah na mashabiki wa soka wamekuwa
wakigawanyika kwa kiasi kikubwa kutambua nani anaweza kutwaa tuzo hiyo.
Tayari De Bruyne, ameshaonyesha hofu yake juu ya mshambuliaji huyo wa
Liverpool anayeongoza kwa kupachika mabao kwa sasa kwenye Ligi Kuu ya
England.
Mbelgiji huyo ameshasema kuwa ana wasiwasi mkubwa kuwa Salah atachukua
tuzo hiyo kutokana na kasi yake tangu alipotua Liverpool mwanzoni mwa
msimu huu.
Salah ni kinara kwa kupachika mabao kwenye ligi hiyo akiwa amefunga
mabao 29 huku akionekana kutawala pia kwenye ligi zote kubwa barani
Ulaya kutokana na mabao mengi aliyofunga.
De Bruyne ambaye amekuwa nguzo sahihi kwenye kikosi cha City msimu huu ambacho kinajiandaa kutwaa ubingwa wa ligi
hiyo ameshasema kuwa itakuwa vigumu sana kwake kumzuia Salah lakini kwa kuwa ni tuzo kila kitu kinawezekana.
Tuzo ambazo zinawania na mastaa hao ni mbili, moja ya mchezaji bora wa
mwaka wa Ligi Kuu England na nyingine ni mchezaji bora wa mwaka wa
waandishi wa habari za soka.
Vita hii imekuja wakati ambapo mastaa hao wawili watakutana kwenye
mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenye Dimba la
Anfield.
Liverpool leo watakuwa wenyeji wa Man City kwenye mchezo huo ambao unaonekana utakuwa mgumu sana kwa timu zote mbili.
“Ndiyo kama mimi ndiye nitapata tuzo ya Mchezaji Bora wa England
litakuwa jambo zuri sana, lakini nafikiri kwanza kwa ajili ya timu.
“Kwa njia moja nafikiri kuwa nastahili kwa kuwa nimekuwa kwenye kiwango kilekile kwa muda mrefu.
“Nina furaha sana mwenyewe na nimekuwa navutika sana kwa jinsi ambavyo nimekuwa nikicheza msimu huu.
“ Nafikiri hakuna mchezo ambao kiwango changu kilikuwa chini, lakini ni
vyema nikawa na hofu na mpinzani wangu kwa kuwa amekuwa bora kwa muda
mrefu na amekuwa mfungaji mzuri, halitakuwa jambo rahisi kuitwaa.
“Salah amekuwa kwenye kiwango cha juu sana kwa kipindi cha hivi karibuni na amecheza vizuri kwenye michezo aliyocheza.
“Kitakwimu ni ngumu kunilinganisha naye, lakini kwa kuwa ni tuzo basi
ngoja tuone mwisho utakuwaje,”alisema kiungo huyo wa City.
De Bruyne ndiye kinara wa pasi kwenye Ligi Kuu ya England na Ulaya kwa
ujumla akiwa amefanikiwa kutoa pasi 15 zilizozaa mabao ambazo ni nyingi
kuliko mchezaji mwingine yoyote msimu huu.
Salah yeye anakwenda kwenye tuzo hiyo akiwa na rekodi nzuri ya kupachika
mabao akiwa ndiye kinara kwa sasa Ulaya nzima baada ya kufunga mabao
29 akifuatiwa na Lionel Messi mwenye mabao 26.
City wanakwenda kwenye Dimba la Anfield, wakitambua kuwa Liverpool
ndiyo imekuwa kizuizi chao msimu huu kwani ndiyo timu pekee ambayo
imefanikiwa kuwafunga kwenye Ligi Kuu England hadi sasa wakiwa
wamepoteza mchezo mmoja tu.
Mbali na kuwafunga Liverpool, wamekuwa kwenye kasi nzuri sana msimu huu
wakiwa wanaamini kuwa wanaweza kumaliza kwenye nafasi ya pili mbele ya
Manchester United ambao nao wamekuwa wakiwania nafasi hiyo.