Wednesday, 4 April 2018
Tuzo ya Mchezaji bora EPL
VITA kubwa kwenye Ligi Kuu ya England sasa imehamia kwenye tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa ligi hiyo ambapo wanaume wawili wanapambana vikali.
Vita hiyo ipo kati ya kiungo wa Manchester City, Kevin De Bruyne, na mshambuliaji wa Liverpool, Mohamed Salah na mashabiki wa soka wamekuwa wakigawanyika kwa kiasi kikubwa kutambua nani anaweza kutwaa tuzo hiyo.
Tayari De Bruyne, ameshaonyesha hofu yake juu ya mshambuliaji huyo wa Liverpool anayeongoza kwa kupachika mabao kwa sasa kwenye Ligi Kuu ya England.
Mbelgiji huyo ameshasema kuwa ana wasiwasi mkubwa kuwa Salah atachukua tuzo hiyo kutokana na kasi yake tangu alipotua Liverpool mwanzoni mwa msimu huu.
Salah ni kinara kwa kupachika mabao kwenye ligi hiyo akiwa amefunga mabao 29 huku akionekana kutawala pia kwenye ligi zote kubwa barani Ulaya kutokana na mabao mengi aliyofunga.
De Bruyne ambaye amekuwa nguzo sahihi kwenye kikosi cha City msimu huu ambacho kinajiandaa kutwaa ubingwa wa ligi
hiyo ameshasema kuwa itakuwa vigumu sana kwake kumzuia Salah lakini kwa kuwa ni tuzo kila kitu kinawezekana.
Tuzo ambazo zinawania na mastaa hao ni mbili, moja ya mchezaji bora wa mwaka wa Ligi Kuu England na nyingine ni mchezaji bora wa mwaka wa waandishi wa habari za soka.
Vita hii imekuja wakati ambapo mastaa hao wawili watakutana kwenye mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwenye Dimba la Anfield.
Liverpool leo watakuwa wenyeji wa Man City kwenye mchezo huo ambao unaonekana utakuwa mgumu sana kwa timu zote mbili.
“Ndiyo kama mimi ndiye nitapata tuzo ya Mchezaji Bora wa England litakuwa jambo zuri sana, lakini nafikiri kwanza kwa ajili ya timu.
“Kwa njia moja nafikiri kuwa nastahili kwa kuwa nimekuwa kwenye kiwango kilekile kwa muda mrefu.
“Nina furaha sana mwenyewe na nimekuwa navutika sana kwa jinsi ambavyo nimekuwa nikicheza msimu huu.
“ Nafikiri hakuna mchezo ambao kiwango changu kilikuwa chini, lakini ni vyema nikawa na hofu na mpinzani wangu kwa kuwa amekuwa bora kwa muda mrefu na amekuwa mfungaji mzuri, halitakuwa jambo rahisi kuitwaa.
“Salah amekuwa kwenye kiwango cha juu sana kwa kipindi cha hivi karibuni na amecheza vizuri kwenye michezo aliyocheza.
“Kitakwimu ni ngumu kunilinganisha naye, lakini kwa kuwa ni tuzo basi ngoja tuone mwisho utakuwaje,”alisema kiungo huyo wa City.
De Bruyne ndiye kinara wa pasi kwenye Ligi Kuu ya England na Ulaya kwa ujumla akiwa amefanikiwa kutoa pasi 15 zilizozaa mabao ambazo ni nyingi kuliko mchezaji mwingine yoyote msimu huu.
Salah yeye anakwenda kwenye tuzo hiyo akiwa na rekodi nzuri ya kupachika mabao akiwa ndiye kinara kwa sasa Ulaya nzima baada ya kufunga mabao 29 akifuatiwa na Lionel Messi mwenye mabao 26.
City wanakwenda kwenye Dimba la Anfield, wakitambua kuwa Liverpool ndiyo imekuwa kizuizi chao msimu huu kwani ndiyo timu pekee ambayo imefanikiwa kuwafunga kwenye Ligi Kuu England hadi sasa wakiwa wamepoteza mchezo mmoja tu.
Mbali na kuwafunga Liverpool, wamekuwa kwenye kasi nzuri sana msimu huu wakiwa wanaamini kuwa wanaweza kumaliza kwenye nafasi ya pili mbele ya Manchester United ambao nao wamekuwa wakiwania nafasi hiyo.
Subscribe to:
Posts (Atom)