TAARIFA KUTOKA OFISI YA TAIFA YA TAKWIMU.
- Hivi karibuni kumekuwa na takwimu zinazotolewa na Kampuni ya GeoPoll yenye Ofisi ya Kanda ya Afrika Mjini, Nairobi Kenya. Takwimu hizo ambazo hutolewa kwa njia ya mitandao ya kijamii, zinahusu ukusanyaji wa taarifa za Televisheni na Redio nchini kwa idadi ya watazamaji na zinatolewa kila baada ya miezi mitatu.
- Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inapenda kuujulisha umma kuwa takwimu hizo sio Takwimu Rasmi (Official Statistics) kwa kuwa hukusanywa kwa mfumo ambao hautambuliwi na NBS kwa mujibu wa kifungu cha 20 cha Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015.
- Takwimu Rasmi kama ilivyofafanuliwa katika kifungu cha 20 cha Sheria ya Takwimu ni takwimu ambazo zimetolewa kwa kufuata Misingi ya utoaji Takwimu Rasmi (Fundamental Principles of Official Statistics) na utolewaji wake umeratibiwa na NBS. Hivyo basi, takwimu zinazotolewa na taasisi au mtu yeyote zitatambuliwa kuwa Takwimu Rasmi iwapo tu zitakidhi vigezo vinavyotolewa na kusimamiwa na NBS.
- Kwa mantiki hiyo, takwimu zinazotolewa na mtu au taasisi yoyote bila kufuata au kukidhi vigezo vinavyotolewa na NBS kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu, hazitambuliwi kuwa ni Takwimu Rasmi na kwa maana hiyo haziwezi kutumika katika kupanga mipango ya maendeleo ya nchi.
- NBS inaitaka Kampuni ya GeoPoll kufuata taratibu zilizoainishwa katika Sheria ya Takwimu, kwa kuwa takwimu zinazotolewa na kampuni hiyo hazijakidhi vigezo vya Takwimu Rasmi na zinapotosha umma na kuleta mkanganyiko kwa wadau pamoja na kuathiri mahusiano ya kiutendaji baina ya vyombo vya habari hapa nchini.
Kuhusu Ofisi ya Taifa ya Takwimu
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) ni taasisi
ya Umma iliyoanzishwa kwa Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2015. Kwa mujibu
wa Sheria hiyo, NBS imepewa mamlaka ya kutoa, kusimamia na kuratibu
upatikanaji wa takwimu rasmi kwa ajili ya matumizi ya Serikali na wadau
wa takwimu.
Aidha, kifungu cha 6 cha Sheria hiyo ya
takwimu, kinaipa NBS jukumu la kutoa na kusimamia Miongozo na Viwango
vya utoaji wa Takwimu Rasmi.
Imetolewa na: Mkurugenzi Mkuu, Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dar es Salaam.
07 Agosti, 2017.
No comments:
Post a Comment