Katika jitihada za kuhakikisha TMA
inashiriki kikamilifu katika kuongeza pato la Taifa, Mamlaka iliandaa
mafunzo ya siku tano ambayo yalikuwa yana lengo la kutoa uelewa wa
sheria, kanuni na taratibu za ununuzi wa umma katika kuboresha utendaji
wa kazi hasa katika usimamizi na utekelezaji wa shughuli za ununuzi na
usimamizi wa mikataba.
Akizungumza wakati akifunga
rasmi mafunzo hayo, Mkurugenzi mkuu wa TMA, Dkt Agnes Kijazi alisema
wakuu wa idara na vitengo wafanye maboresho kwenye maeneo yaliyokuwa
na changamoto na kitengo cha ununuzi waboreshe utendaji wa kazi sambamba
na kusimamia vizuri taratibu zote zinazohusu ununuzi kwa mujibu wa
sheria na kanuni zake, kama ilivyoelekezwa na washauri waelekezi kutoka
PSPTB ili kuisaidia Mamlaka yetu kutekeleza sera na mikakati ya Serikali
ya kupunguza gharama za ununuzi kwa lengo la kuboresha pato la Taifa.
Aidha Dkt. Kijazi aliishukuru
Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) kwa kukubali kutoa wataalam
katika upande wa sheria ya ununuzi na kuahidi kuendelea kushirikiana na
Bodi hiyo kila inapobidi.
Kwa upande wa Bodi ya utaalam
wa ununuzi na ugavi Mkurugenzi wa Fedha na Utawala Bwana Paul Bilabaye
kwa niaba ya Mtendaji Mkuu alitoa pongezi kwa TMA kwa uamuzi wa kutoa
mafunzo haya kwa Viongozi wanaohusika na utekelezaji wa Sheria ya
Ununuzi na Ugavi.
Mafunzo haya yamejenga uwezo
kwa Idara tumizi, Kamati za tathmini, Kitengo cha Ununuzi na Ugavi
pamoja na Bodi ya Zabuni katika kutekeleza majukumu yake.
Mafunzo hayo ya siku tano
yamefanyika katika ukumbi wa mikutano, Makao Makuu ya TMA, Ubungo Plaza
na kuhudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu, Wakuu wa idara na wakuu wa vitengo
vyote pamoja na wajumbe wa Bodi ya Zabuni ya Mamlaka ya Hali ya Hewa.
Imetolewa na
Ofisi ya Uhusiano
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA
No comments:
Post a Comment