Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Tulia Ackson akiongoza kikao cha nne cha
Mkutano wa saba wa Bunge la 11 linaloendelea Mjini Dodoma.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais TAMISEMI Mhe. Suleimani Jafo akijibu hoja mbalimbali za wabunge
katika kikao cha nne cha Mkutano wa saba wa Bunge la 11 linaloendelea
Mjini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe.
Dkt. Philip Mpango akijibu hoja mbalimbali za wabunge katika kikao cha
nne cha Mkutano wa saba wa Bunge la 11 linaloendelea Mjini Dodoma.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi
Mhe. Mwigulu Nchemba akijibu hoja mbalimbali za wabunge katika kikao cha
nne cha Mkutano wa saba wa Bunge la 11 linaloendelea Mjini Dodoma.
Mbunge wa Viti maalum Morogoro
(CHADEMA) Mhe. Devotha Minja akitoa hoja Bungeni katika kikao cha nne
cha Mkutano wa saba wa Bunge la 11 linaloendelea Mjini Dodoma.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi
Mhe. Mwigulu Nchemba(kulia) na Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsi
Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu wakifuatilia kikao cha nne cha Mkutano
wa saba wa Bunge la 11 linaloendelea Mjini Dodoma.
Picha zote na Raymond Mushumbusi MAELEZO Dodoma.
SERIKALI YAFAFANUA UINGIZAJI WA
MAYAI KUTOKA NJE, MAPAMBANO DHIDI YA KIFUA KIKUU NA MASHIRIKA NA TAASISI
ZA UMMA KUJIUNGA NA NHIF.
Dodoma,Jumatatu, 10 April, 2017.
Serikali imefafanua kuhusu
uingizaji wa mayai kutoka nje, mapambano dhidi ya kifua kikuu na
mashirika na taasisi za umma kujiunga na Mfuko wa Bima wa Taifa na
utaratibu wa michezo ya bahati nasibu hapa nchini. Ufafanuzi huo
umetolewa leo mjini hapa.
Zuio la Uingizaji wa Mayai kutoka Nje.
Serikali imesema kuwa hakuna
mwekezaji yeyote aliyeruhusiwa kupewa kibali cha kuingiza vifaranga au
mayai ya kuku nchini kwa ajili ya biashara.
Katika kusimamia hili, kuanzia mwaka 2013 hadi 2017 vifaranga 67500 vilivyoingizwa nchini kinyume na sheria viliteketezwa.
Akifafanua kuhusu hoja hiyo,
Naibu Waziri wa Kilimo,Mifugo na Uvivu, Mhe.William Ole Nasha amesema
wako wawekezaji wachache ambao hupewa vibali maalum vya kuingiza mayai
au vifaranga wa kuku wazazi(Parent Stock) tu na ukaguzi kwa ajili ya
kudhibiti uingizaji vifaranga na mayai unaendelea na hatua kali
zinachukuliwa kwa yeyote anayekamatwa kwa kukiuka utaratibu.
Mapambano dhidi ya kifua kikuu na Silicosis
Serikali imesema kuwa
inafahamu changamoto ya uwepo wa magonjwa ya kifua kikuu na Silicosis
katika maeneo ya wachimbaji wa Madini. Kwa upande wa Kifua Kikuu
inakadiriwa kuwa tatizo hilo ni kubwa ikilinganishwa na hali halisi
katika maeneo mengi.
Kwa upande wa Silicosis
kumekuwepo na ripoti za wagonjwa wachache katika hospitali za Serikali
ikiwemo Kibong’oto ambao ni wachimbaji wadogo wadogo wa madini.
Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo
ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt. Khamis Kingwangalla amesema
Serikali kupitia Halmashauri zilizo katika maeneo ya migodi imeanza
kuweka mikakati ya kudhibiti magonjwa haya na pia kutoa elimu kwa
wachimbaji namna ya kujikinga na vumbi na kutumia njia sahihi za
uchimbaji.
Ameongeza kuwa Serikali
itaongeza wigo wa huduma katika vituo vya afya kwenye maeneo
yaliyoathirika, hususan Mkoa wa Geita ili vituo viwe na uwezo wa
kuchunguza na kutibu magonjwa hayo na kuwajengea uwezo wataalamu wa Afya
katika kuhudumia wagonjwa katika maeneo ya migodi.
Mashirika na Taasisi za Umma kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Serikali imesema kuwa hadi
kufikia tarehe 31/12/2016, Idara za Serikali,Taasisi na Mashirika ya
Umma zinazotumia Huduma za Bima ya Afya za NHIF zimefikia 307.
Naibu Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto, Dkt. Khamis Kingwangalla
amesema Mashirika, Taasisi na Idara za Serikali ambazo hazijajiunga na
Mfuko huo zipo 23 zikiwemo TRA, BOT, TANESCO, NHC, TPA,PSPF, LAPF, PPF,
EWURA, NCA, na GEPF.
Ameongeza kuwa Mfuko huo
unaendelea na jitihada za kukutana na uongozi wa Mashirika hayo ya umma
kwa lengo la kutoa elimu na kuwahimiza juu ya umuhimu wa kujiunga kama
ilivyoainishwa katika Sheria ya Mfuko.
Aidha, hadi kufikia mwezi
Machi,2017 idadi ya wanachama katika Mfuko huo imefikia wanachama 792987
kutoka wananchama 474760 mwaka 2012.
Imetolewa na:
Idara ya Habari-MAELEZO.
No comments:
Post a Comment