Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limetoa nafasi ya pili na ya
mwisho kwa ajili ya mchakato wa kuwapata wawakilishi wawili wa Tanzania
katika Bunge la Afrika Mashariki kupitia Chama cha Demokrasia na
Maendeleo.
Akitoa taarifa yake bungeni leo , Spika wa Bunge hilo Job Ndugai amesema
hadi sasa nafasi hizo bado ni za CHADEMA na atahakikisha haki hiyo
wanaipata na kwamba Katibu wa Bunge atatoa taarifa ni lini mchakato huo
utafanyika
Katika hatua nyingine, Ndugai ametoa tahadhari kwa chama hicho kuwa yeye
ndiye mwenye mamlaka ya kutoa utaratibu wa kupatikana kwa wawakilishi
wa Tanzania kupitia vyama vya upinzani, hivyo endapo wasipotumia nafasi
hiyo, atatumia mamlaka aliyonayo kutangaza utaratibu mwingine ili
Tanzania isikose wawakilishi katika nafasi hizo.
“Ikumbukwe kuwa maamuzi haya ya kuwatenganisha wabunge wa upinzani
kwa kuangalia vyama vyao ni maamuzi ya Spika, tukumbuke mabunge
yaliyopita maspika wenzangu hawakufanya hivyo, waliwaweka wabunge wote
wa upinzani kwenye kundi moja, mimi nikasema twende na demokrasia hii ya
wawili, ambayo katika kufanya hivyo, mimi yuleyule,tuendelee.
Hatuwezi kukubali nchi yetu ikose uwakilishi nchi yetu ikatekwa nyara
kwa sababu fulani fulani". Amesema Ndugai
Pia Ndugai amewatoa hofu watanzania kuwa hawatakosa uwakilishi kwa kuwa
anajua cha kufanya. "Tutatoa nafasi ya pili, lakini baada ya nafasi ya
pili, tunajua hatua itakayofuata, nawahakikishia watanzania kwamba
hawatakosa nafasi katika bunge hilo”
Katika uchaguzi uliofanyika juzi, Bunge hilo liliwachagua wajumbe 7 kati
ya 9 waliohitajika, huku wagombea wawili wa CHADEMA Ezekiah Wenje na
Lawrence Masha wakikataliwa kwa kupigiwa kura za hapana.
No comments:
Post a Comment