- Kutoka ngazi ya Kidiplomasia hadi ushirikiano wa kiuchumi na kijamii
- Zasaini mikataba mitatu ya ushirikiano
Ziara ya hivi karibuni ya
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia
Hailemariam Dessalegn nchini Tanzania, imefungua ukurasa mpya wa
uhusiano na ushirikiano baina ya nchi hizo mbili. Mwandishi Said Ameir
wa Idara ya Habari- MAELEZO anaelezea zaidi.
Hii ni ziara ya pili kwa
Waziri Mkuu Dessalegn kuifanya nchini Tanzania ambapo mara ya kwanza
ilikuwa mwezi Novemba 2015, kwa mwaliko wa Rais wa wakati huo Jakaya
Mrisho Kikwete. Alikuja kushuhudia uzinduzi wa kiwanda cha kutengeneza
madawa ya kuulia viluilui vya ugonjwa wa malaria huko Kibaha mkoa wa
Pwani.
Safari hii, ziara ya Waziri
Mkuu huyo imebadili kabisa upepo wa uhusiano kati ya nchi yake na
Tanzania kwa kuupeleka uhusiano huo kutoka ngazi ya kisiasa na
kidiplomasia kwenda katika ngazi ya ushirikiano wa kiuchumi na kijamii.
Ni ziara inayotokana na
mwaliko wa Rais John Pombe Magufuli alioutoa kwake wakati wa Mkutano wa
Kilele wa Viongozi na Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika uliofanyika
mjini Adis Ababa, Ethiopia mwanzoni mwa mwaka huu ambapo viongozi hao
wawili walipata fursa ya kufanya mazungumzo ya faragha.
Kwa miaka mingi kumekuwepo na
ziara za mara kwa mara za Watendaji Wakuu na Viongozi wa ngazi za juu
wa Serikali zikiwa na lengo la kuendeleza uhusiano na urafiki kati yake.
Marais wote wastaafu wa Tanzania wamewahi kufanya ziara rasmi nchini
Ethiopia mbali ya ziara za kikazi za kuhudhuria Vikao vya Viongozi na
Wakuu wa Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU).
Ziara ya Waziri Mkuu
Dessalegn ilimalizika kwa kushuhudia kutiwa saini kwa mikataba mitatu
muhimu ya ushirikiano ambayo itabadili sura na taswira ya uhusiano kati
ya nchi mbili hizi.
Mkataba wa kwanza ni wa
kuanzisha Tume ya Pamoja na Ushirikiano kati ya Tanzania na Ethiopia
ambao unaweka msingi madhubuti wa ushirikiano kati ya nchi hizo huku
ukitoa fursa kwa pande hizo kuangalia maeneo mapya ya ushirikiano kwa
faida ya nchi hizo na wananchi wake.
Makubaliano mengine yalihusu
kukabiliana na tatizo la uhamiaji haramu ambalo ni moja kati ya matatizo
makubwa barani Afrika hivi sasa, ushirikiano katika Biashara, Uwekezaji
na vita dhidi ya ugonjwa wa malaria.
Tanzania na Ethiopia
zilikubaliana pia kushirikiana katika Sekta ya Utalii ambapo nchi zote
zimekuwa zikifanya vyema katika sekta hiyo. Chini ya makubaliano hayo
nchi hizo zitabadilishana uzoefu na mafunzo pamoja na kuhimiza uwekezaji
katika sekta hiyo.
Katika kuhakikisha kuwa
uhusiano huu haubaki kwa vingozi na serikali pekee, nchi hizi
zimekubaliana kuondoa VIZA za kuingia na kutoka kwa Wananchi wa nchi
zao. Hatua hii inakusudia kuondoa vikwazo na kurahisisha safari za
kitalii, biashara na pia kuhamasisha uwekezaji.
Kitu muhimu ambacho
kimeonekana katika ziara hii ni utayari wa viongozi hawa wawili na
dhamira ya dhati waliyo nayo katika kuimarisha ushirikiano kati ya nchi
zao. Wameonesha na kutambua haja ya kuimarisha ushirikiano katika
kukabiliana na changamoto zinazozikabili nchi na wananchi wao.
Wanaamini kuwa nchi za Afrika
zina uwezo wa kuondokana na kadhia ya umasikini na uduni wa maendeleo
endapo zitatambua uwezo wao, kuainisha kwa umakini mkubwa vipaumbele vya
maendeleo na kushirikiana kutumia rasilimali ilizo nazo kujiletea
maendeleo. Viongozi hao wameikumbatia ile dhana ya ‘suluhisho la
matatizo ya Afrika ni Afrika yenyewe’.
Halikadhalika, kauli ya
Waziri Mkuu wa Ethiopia kuwa nchi za Afrika zisiwe washindani bali
washirika ni kauli thabiti na endapo ikitekelezwa kwa dhati na umakini
italisaidia bara la Afrika kujikwamua na matatizo yake yanayolisibu kwa
miongo mingi sasa.
Kwa kuonesha mfano wa
utekelezaji kwa vitendo kauli hiyo, Waziri Mkuu huyo alitoa ahadi ya
nchi yake kulisaidia Shirika la Ndege la Tanzania-ATCL ili liweze
kufanya vizuri kama lilivyo kwa Shirika la Ndege la nchi yake (Ethipian
Airline).
Aidha, mkakati wa kukifanya
Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) kuwa kituo
chake kikuu cha mizigo kwa Afrika pamoja na nchi yake kuamua kuitumia
bandari ya Dar es Saalaam ni miongoni mwa hatua zinazodhihirisha dhamira
ya kweli ya kuimarisha ushirikiano miongoni mwa nchi za bara la Afrika.
Ni jambo la kufurahisha kuona
kuwa ziara hii pia imezipa nguvu jitihada za kuimarisha lugha ya
Kiswahili kuwa lugha ya Afrika ambapo Waziri Mkuu wa Ethiopia aliahidi
kuteua Chuo Kikuu kimoja nchini kwake kufundisha lugha hiyo.
Kwa upande wake Rais Magufuli
aliunga mkono hatua hiyo kwa kuahidi kutoa Walimu wa kufundisha. Hiyo
ni hatua muhimu katika kuimarisha matumizi ya lugha ya Kiswahili barani
Afrika.
Tanzania na Ethiopia zina
mambo mengi ya kujifunza kila upande kuanzia uendelezaji wa Sekta ya
kilimo, mifugo, uzalishaji wa nishati na hata katika michezo.
Wakati Tanzania inafanya
vizuri katika kilimo, Ethiopia nayo inafanya vizuri katika Sekta ya
mifugo hasa katika viwanda vya ngozi. Nchi mbili hizi ndizo zinazoongoza
kwa idadi kubwa ya mifugo barani Afrika, Ethiopia ikiwa ya kwanza,
ikifuatiwa na Tanzania.
Kwa hivyo, Tanzania ina mengi
ya kujifunza kutoka Ethiopia katika Sekta hii kwa minajili ya kuongeza
thamani za bidhaa za ngozi kwa kuanzisha viwanda na kutengeneza bidhaa
badala ya kuuza ngozi ghafi nchi za nje. Ethiopia nayo inacho cha
kujifunza kutoka Tanzania katika Sekta ya kilimo.
Ni kweli ulio wazi kuwa nchi
haziwezi kuwa tajiri kwa kuuza sehemu kubwa ya malighafi zake kwenye
masoko ya dunia ambapo daima bei hupangwa na wanunuzi wenyewe ambao ni
mataifa tajiri. Kwa hiyo hatua za viongozi hao kudhamiria kushirikiana
kuhakikisha nchi zao zinahamasisha ujenzi wa viwanda vitakavyotumia
malighafi hususan bidhaa za kilimo ni hatua nzuri ya kujivunia.
Ndio maana waliuliza swali;
ikiwa Ulaya imeweza, Asia imeweza, kwa nini Afrika isiweze? Swali hili
linafunganisha upeo wa juu wa mtazamo chanya wa maendeleo na uthubutu
ulioambatana na dhamira ya kweli ya kuleta maendeleo na kuondokana na
umasikini.
Katika ile dhana ya Afrika
kutumia kila rasilimali zake kujikwamua, Tanzania inaweza kujifunza
kutoka Ethiopia juu ya namna ya kuwashirikisha Watanzania walio
ughaibuni (diaspora) katika kuleta maendeleo ya humu nchini.
Ni kweli kwa zaidi ya miaka
15 sasa, zimekuwepo jitihada za makusudi za kuwahamasisha Watanzania hao
kushiriki katika kusukuma gurudumu la maendeleo lakini ushiriki wao
bado haujafikia kiwango kama ilivyo kwa nchi nyingine kama Ethiopia.
Wana-diaspora wa Ethiopia
wanatoa mchango mkubwa katika kuleta maendeleo nchini mwao na wamekuwa
chachu katika kuimarisha uwekezaji kwa kuvutia wageni (wawekezaji) na
uhaulishaji wa tekinolojia kutoka nchi zilizoendelea kwenda nchini
Ethiopia. Kwa hiyo, ushirikiano huu ni fursa nyingine kwa Tanzania
kujifunza kutoka kwa mshirika wake huyo.
Hakuna shaka yeyote kuwa
kutiwa saini kwa mikataba hiyo mitatu ya ushirikiano kati ya nchi hizo
mbili kumefungua ukurasa mpya katika historia ya uhusiano baina yake.
Mikataba hiyo inatoa fursa kwa nchi hizo sio tu kujenga misingi imara ya
ushirikiano katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii bali pia
kusaidiana kutafuta suluhisho la changamoto za kimaendelo
zinazozikabili.
Kutiwa saini kwa mikataba
hiyo na ahadi mbalimbali za ushirikiano zilizotolewa na Waziri Mkuu wa
Ethiopia ni kipimo kingine kinachodhihirisha namna ambavyo hatua kwa
hatua Rais Magufuli anavyozidi kung’ara katika medani za diplomasia na
siasa za Kimataifa.
Rais Magufuli amezidi kuwa na
ushawishi na kuzidi kuaminika miongoni mwa viongozi wenzake wa nchi
mbalimbali pamoja na wadau wa maendeleo. Ameimarisha siasa ya nje ya
Tanzania kwa staili ya ‘hapa kazi tu’ kwa kujipambanua kuwa ni kiongozi
mwenye msimamo na anayetetea kile anachokiamini kwa vitendo si kwa
maneno matupu. Kwa hivyo, ni matumaini ya Wananchi wa Tanzania na
Ethiopia kuona makubaliano yaliyofikiwa na viongozi wao yanatekelezwa
ili kukidhi matarajio yao.
No comments:
Post a Comment