Jovina Bujulu- MAELEZO.
Kila mwaka ifikapo Machi 8 kila
mwaka, wanawake duniani kote huadhimisha siku yao ambapo hujitathmini
kupitia shughuli mbalimbali za maendeleo walizofanya, changamoto
zilizopo na kuweka mikakati ya utatuzi wa changamoto hizo.
Akiongea hivi karibuni katika
kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, Katibu mkuu wa Wizara
ya Afya na Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bi Sihaba Nkinga
alisema kuwa kauli mbiu ya mwaka huu inasema “Tanzania ya Viwanda;
Wanawake ni Msingi wa Mabadiliko”
Kauli mbiu hii inasisitiza
kuwajengea wanawake uwezo wa kitaaluma, kibiashara, upatikanaji wa
mitaji, masoko na biashara ili waweze kushiriki kwa usawa, na kunufaika
na fursa zilizopo badala ya kuwa wasindikizaji.
“Ujumbe wa kauli mbiu hii
umezingatia sera ya maendeleo ya wanawake na jinsia ya mwaka 2000 na
ajenda ya 2030 ya maendeleo endelevu hususani lengo namba 5 kuhusu usawa
wa jinsia na uwezeshaji wanawake kiuchumi” alisema Bi Nkinga.
Kauli mbiu ya mwaka huu
imetotolewa kutokana na kauli mbiu ya Umoja wa Mataifa (UN) isemayo
“Uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi katika Dunia ya Mabadiliko ya Kazi”.
Akizungumza hivi karibuni,
Mkurugenzi wa Chama cha Wanahabari Wanawake nchini (TAMWA) Mama Edda
Sanga alisema kuwa wanawake wanapaswa kujiwezesha katika maeneo ya
kiuchumi, kisiasa, na kijamii ili wapate fursa ya kushiriki katika
maamuzi mbalimbali ambayo hatimaye yatawaletea tija na mafanikio.
Hii ina maana kuwa, endapo
wanawake watapata nafasi ya kushiriki katika maamuzi mbalimbali ni
rahisi kwao kusikilizwa na hata kuwa na sauti katika masuala ya wao
kumiliki ardhi, majumba na hata viwanda.
Aidha, kauli mbiu hii
inawahamasisha wanawake kuhakikisha kuwa kunakuwa na usawa wa jinsia
unaoondoa vikwazo na kuhakikisha wanapata fursa sawa na kuweka
ulinganifu katika ushiriki ambao unawanufaisha kiuchumi kuanzia ngazi ya
familia.
Ili kufikia malengo ya kujikomboa
kiuchumi, wanawake wanatakiwa kujitambua na pia kutambua malengo na
mipango yao. Wanatakiwa kutambua na kutumia fursa vizuri wanayopata hasa
mahali watakapopata taarifa za kuwanufaisha kiuchumi kwa mfano benki,
vikundi vya mikopo, taasisi au hata kwa watu binafsi.
Kumekuwa na juhudi mbalimbali za
kuwakwamua wanawake kiuchumi, kutoka kwenye taasisi, mashirika na watu
binafsi, hata hivyo wao pia wanahitaji kujikomboa kwa kutumia juhudi
zao binafsi kama vile kujiunga katika vikundi waweze kukopeshwa ili
waweze kujiajiri katika mkondo wa uzalishaji mali, kama vile kuanzisha
viwanda vidogo vidogo, kwa mfano viwanda vya usindikaji vyakula, kazi za
mikono na ushonaji ambavyo havihitaji mtaji mkubwa.
Hii itawafanya kunufaika na kuondoa hali ya utegemezi katika jamii, na hivyo kujiondoa katika hali ya unyonge.
Ni ndhahiri wanawake ndio
wazalishaji wakubwa katika nyanja za kiuchumi, hivyo katika kutimiza
ndoto na malengo zao ni budi juhudi zitumike ili washiriki katika kukuza
pato lao na taifa kwa ujumla.
Naye Bibi Lilian Liundi ambaye ni
Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) anasema kuwa katika
kusherekea siku ya wanawake duniani, taasisi yao ilifanya kongamano
hivi karibuni pamoja na mambo mengine walizungumzia mpango wa taifa
kuhusu ushiriki wa wanawake katika kuelekea uchumi wa viwanda vya kati.
Alisema kuwa wanawake wa mjini
kwa sasa wanashiriki vizuri katika shughuli ambazo huwaongezea kipato
wakati wanawake wa vijijini ushiriki wao katika shughuli za kuwaongezea
kipato si wa kuridhisha kwani wanatumia muda mrefu kutembea kutafuta
maji na kuni kwa ajili ya matumizi ya familia.
Bibi Liundi alitoa wito kuwa
huduma za jamii zisogezwe karibu na jamii ili wanawake ambao ni
wazalishaji mali wakubwa wapate muda wa kutosha kushiriki katika
shughuli za kujiongezea kipato badala ya kutembea umbali mrefu kufuata
huduma hizo.
Naye Bibi Magreth Dotto ambaye ni
Mhandisi wa Migodi, na Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo Kikuu cha
Dar-es-salaam aliwashauri watoto wa kike kusoma masomo ya sayansi kwa
kuzingatia kasi ya ukuaji wa teknolojia kila siku ili baadaye wapate
nafasi nzuri katika jamii na kutoa mchango wao katika kutatua changamoto
za kijamii na taifa.
“Uhandisi unawezekana kwa
wasichana na ni taaluma nzuri, hivyo wasichana waache kuyaogopa masomo
ya sayansi, ni taaluma inayobadilisha maisha kwa kuyaboresha kwa sababu
inalipa vizuri” alisema Bibi Magreth.
Kwa upande wake Dkt. Ave Maria
Samakafu ambaye ni Mhadhiri katika Chuo cha Sayansi ya Tiba Muhimbili na
Mratibu wa Taifa wa Taasisi ya Wanawake ya Ulingo alisema kwa sasa
wanawake wana mwamko mkubwa ambao umeleta mageuzi katika familia na
kuinua kipato chao.
“Kwa sasa tunaona ushiriki mkubwa
wa wanawake katika nyanja ya uchumi kwa sababu kuna wanawake
wafanyabiashara wadogowadogo, wa kati na hata wakubwa” anasema Dkt
Semakafu.
Alisema kuwa elimu inahitajika
zaidi kwa wanawake wa vijijini ambao bado wanatawaliwa na tafsiri potofu
ambapo ukandamizaji wa wanawake bado unapewa nafasi kubwa na jamii,
hivyo kuwafanya wasisonge mbele katika kujiletea maendeleo yao.
Dkt. Semakafu aliendelea kusema
kuwa wanawake wengi wa mjini wanatambua nafasi zao katika jamii, hivyo
wanatumia ufahamu huo kama fursa kwao ambazo zinawasaidia katika kuleta
mageuzi ndani ya familia zao.
“Vijana wa kike wamekuja na nguvu
mpya, kinachoendelea sasa hivi kinafungua uelewa wa jamii, watoto na
wazazi na kuwafanya watambuliwe na jamii” alisema Dkt. Semakafu.
Dkt. Semakafu alitoa mfano
unaodhihirisha nafasi ya mwanamke akimtaja Agnes Magongo ambaye hivi
karibuni ameshinda tuzo ya UN ya “women economic empowerment” ambayo ni
tuzo ya uwezeshaji wa wanawake.
“Wanawake tushiriki katika
kuboresha maisha yetu, tusiwe wasindikizaji bali watendaji, twende
pamoja katika uchumi wa viwanda ili tuweze kumiliki viwanda” alimalizia
Dkt. Semakafu.
Katika kuhimiza fursa za uchumi
kwa wanawake kauli mbiu ya mwaka huu inalenga kuhamasisha jamii na wadau
wote nchini kuongeza fursa za kiuchumi kwa wanawake ili waweze
kushiriki na kunufaika nazo hasa kipindi hiki ambapo Tanzania inaelekea
azma ya uchumi wa kati kwa misingi ya kuwa nchi ya viwanda.
Mama Sihaba aliwakumbusha wadau
wote katika ngazi zote kuweka mikakati thabiti ya kutatua changamoto
zinazokwamisha kufikiwa kwa usawa wa jinsia na kusababisha wanawake na
wasichana kushindwa kutimiza malengo na ndoto zao kimaisha.
No comments:
Post a Comment