WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
akisalimiana na mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania nje ya nchi baada ya
kuzungumza nao Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam, Februari 7, 2017
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa akiwa
katika picha ya pamoja na mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi
mbalimbali baada ya kuzungumza nao Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam,
Februari 7, 2017. Kutoka kushoto ni Samwel Shelukindo (Ufaransa), Dkt.
James Msekela (Uswisi), Mbelwa Kairuki (China), Paul Mella (DRC), Dkt.
Emmanuel Nchimbi (Brazil) George Madafa (Italy) na Elizabeth Kiondo
(Uturuki). (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
akizungumza na mabalozi ambao wanaiwakilisha Tanzania nje ya nchi na
wanatarajiwa kuripoti kwenye vituo vyao vya kazi hivi karibuni, Ofisini
kwake Jijini Dar es Salaam, Februari 7, 2017 (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
amewataka mabalozi wa Tanzania katika nchi mbalimbali kuhakikisha
wanatumia uwakilishi wao kutafuta wawekezaji watakaokuja kuwekeza katika
sekta ya viwanda nchini.
Amesema mkakati wa Serikali ni
kuimarisha uchumi hadi wa kati kupitia sekta ya viwanda, hivyo jukumu
la mabalozi hao ni kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo
(Jumanne, Februari 7, 2017) alipokutana na mabalozi wa wanaoiwakilisha
Tanzania katika nchi za Uturuki, Brazil, China, Italy, Ufaransa,
Jamuhuri ya Kidemkrasi ya Congo (DRC) na Uswisi.
Mabalozi hao ni Balozi Dk.
Emmanuel Nchini (Brazil), Balozi Elizabeth Kiondo (Uturuki), Balozi
George Madafa (Italy), Balozi James Msekela (Uswisi),Balozi Samuel
Shelukindo (Ufaransa), Balozi Paul Mella (DRC), Balozi Mbelwa Kairuki
(China).
“Serikali inahitaji watu wa kuja
kuwekeza katika viwanda ili kuongeza thamani ya mazao kabla ya kuyauza
nje ya nchi, hivyo jukumu lenu ni kuhakikisha tunapata wawekezaji wenye
sifa,” amesema.
Pia Waziri Mkuu amewataka
mabalozi hao kutumia uwakilishi wao katika nchi hizo kwa kuhakikisha
wanatangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini ili kuongeza idadi ya
watalii wanaokuja Tanzania.
Aidha, Waziri Mkuu amewataka
mabalozi hao kulinda maslahi ya Taifa katika nchi hizo ikiwa ni pamoja
na kuimarisha uhusiano uliopo kati ya Tanzania na mataifa hayo.
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu amewataka mabalozi hao kuhakikisha wanawatambua Watanzania
wanaoishi katika mataifa hayo na kushirikiana nao katika kutafuta
wawekezaji wa kuja kuwekeza nchini.
Kwa upande wake Balozi Mella
ambaye alizungumza kwa niaba ya mabozi wenzake alimuhakikishia Waziri
Mkuu kwamba watakwenda kutekeleza wajibu wao ipasavyo.
No comments:
Post a Comment