Tuesday, 7 February 2017

Serikali kudhibiti matumizi holela ya fedha za kigeni

PIX-4-6
Serikali imesema kuwa katika kudhibiti matumizi holela ya fedha za kigeni, Benki Kuu kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania imeongeza usimamizi katika maduka ya kubadilishia fedha za kigeni ambapo taarifa za kila muamala wa fedha za kigeni unaofanywa zinapaswa kuoneshwa.
Kauli hiyo imetolewa Bungeni leo na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt Ashatu Kijaji, wakati akijibu maswali ya Mbunge wa Igunga Mhe. Dalaly Peter Kafumu aliyetaka kupewa ufafanuzi juu ya Kwanini Serikali isidhibiti matumizi holela ya dola nchini ili kupunguza utakasishaji wa fedha na kuimarisha ukuaji wa uchumi kama zinavyofanywa nchi nyingi duniani.
Aidha, Dkt Kijaji alifafanua hatua zimechukuliwa pia kuhakikisha kuwa miamala ya fedha za kigeni inayofanywa na mabenki ni ile inayohusu shughuli za kiuchumi tu ili kulinda thamani ya shilingi. 
Vilevile, tamko na mwongozo uliotolewa na Serikali mwaka 2007, ulieleza kuwa bidhaa na huduma zinazowalenga watalii au wateja wasio wakazi wa Tanzania, bei zake zinaweza kunukuliwa kwa sarafu mbili, yaani shilingi ya kitanzania na sarafu ya kigeni na malipo kufanyika kwa sarafu ambayo mlipaji atakuwa nayo. Pia, mkazi yeyote wa Tanzania asilazimishwe kulipia bidhaa au huduma yoyote hapa nchini kwa fedha za kigeni.
“Msingi wa kuruhusu soko huru la fedha za kigeni hapa nchini ni hatua ya makusudi ambayo ilichukuliwa na Serikali ili kuiwezesha nchi kuondokana na hali ya kuadimika kwa fedha za kigeni ilikuwa dola za Kimarekani milioni 4,093.7 wakati amana za fedha za kigeni za wakazi wa Tanzania zilikuwa dola za Kimarekani milioni 2,933.1 na rasilimali za fedha za kigeni za mabenki zilikuwa kiasi cha dola za Kimarekani milioni 1,021.1” alisema Dkt. Kijaji.
Dkt Kijaji ameeleza kuwa Tanzania ina urari wa biashara ya nje ambao umetokana na sera huru za kigeni, ambazo zimechangia kuimarisha uchumi kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita, wastani wa ukuaji wa uchumi wa Taifa letu katika kipindi cha miaka kumi iliyopita ulikua ni asilimia 7, ikiwa ni wastani wa juu sana ikilinganishwa na  nchi nyingine duniani. 
“Mfano, wastani wa ukuaji wa uchumi wa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara ni asilimia 5.4 katika kipindi hicho wakati ule wa nchi zinazoibukia kiuchumi ulikua ni asilimia 5.8” alisisitiza Dkt. Kijaji
Alisema kuwa njia zinazotumika kutakatisha fedha ni pamoja na kuziingiza haramu kwenye taasisi za fedha na kuziwekeza katika rasilimali halali kama ardhi na nyumba. Baadhi ya mambo yanayowapatia wahalifu fedha haramu ni pamoja na biashara ya dawa za kulevya, rushwa, ujangili, ujambazi, ukwepaji kodi n.k. Aidha fedha zinazotokatana na shughuli za kihalifu zinaweza kuwa shilingi za Kitanzania, dola za Kimarekani au fedha nyingine yoyote ile. 
Naibu Waziri huyo wa Fedha na Mipango amesema ziko kanuni ambazo zinafuatwa na vyombo vya fedha ili kuzuia utakatishaji wa fedha zote zilizopatikana kutoka vyanzo haramu na sio dola pekee huku akibainisha kuwa Benki Kuu ya Tanzania ina jukumu la usimamizi wa taasisi za fedha, hufuatilia mabenki ili kuhakikisha kuwa kanuni hizo zinafuatwa.

No comments:

Post a Comment