Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Justo
Lyamuya akitoa tathimini ya upimaji Ardhi nchini kwa waandishi wa
Habari ( hawaonekani pichani) Kushoto kwake ni Mkurugenzi Msaidizi
upimaji na Ramani; Simon Katambi na Kulia kwake ni Mkuu wa Kitengo cha
Mawasiliano Serikalini; Mboza lwandiko
Viwanja 32,303 na mashamba 76
yamepimwa nchini toka robo ya kwanza ya mwaka / Julai – Septemba 2016,
kwa maazimio ya upimaji wa vipande 400,000 vya Ardhi ifikapoJuni, 2017.
Akitoa taarifa kwa Vyombo vya habari;
Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi; Justo Lyamuya ameeleza. Alisema, toka mwaka 1961 hadi 2016
vimepimwa viwanja 1,359,899 na mashamba 24,579. Kwa kipindi cha miaka 6
iliyopita kuanzia 2010 hadi Juni 2016 vimepimwa viwanja 558,403 na
mashamba 4,314.
Bw. Lyamuya alitoa ufafanuzi wa upimaji uliofanyika wa maeneo mbalimbali nchini. Alieleza Upimaji wa ardhi chini ya maji (Hydrographic Survey)
umefanyika kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo kwa ushirikiano na
Jeshi la majini la India, kufuatia makubaliano kati ya serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya India tumeweza kupima
bandari za Dar es Salaam, Zanzibar na Mkoani Pemba. Ramani za Bandari
hizo zipo kwenye duka la ramani tayari. Mwaka huu upimaji wa bandari ya
Tanga umefanyika na kazi ya uwandani imekamilika na ile ya ofisini
inaendelea.
Katika eneo la Upimaji Mipaka ya Vijiji; Alisema kuwa vijiji 10,667 kati ya vijiji 12,000 vimepimwa. Chini ya Mradi wa Land Tenure Support Programme umepima vijiji 52 kwenye wilaya 3 za Morogoro (Kilombero, Malinyi na Ulanga).
Katika Upimaji wa usimikaji alama za
Msingi za Upimaji, alieleza kuwa; Alama za msingi za upimaji zimesimikwa
nchi nzima zikiwa katika viwango tofauti. Zero order zipo 16, First
Order zipo 72 na second order 525. Baadhi ya maeneo alama hizi
zimesambazwa katika umbali utakaoruhusu upimaji kufanyika kwa urahisi.
Sambamba na usambazaji huo wa alama za upimaji; umbo la dunia (Tanzania Geoid) limekokotolewa kurahisisha upatikanaji wa vipimo vya miinuko.
Vile vile, katika eneo la Upimaji Mipaka
ya Kimataifa, Bwn. Lyamuya alisema; “Kwa mipaka ya kimataifa mipaka yote
ya baharini na majirani zetu imeandaliwa Mikataba ya makubaliano na
kuridhiwa. Kwa upande wa Maziwa makubaliano ya uwekaji mpaka ndani ya
Ziwa Tanganyika Kati ya Tanzania, DRC, Zambia na Burundi, yamefikiwa.
Utekelezaji utaendelea baada ya fedha kupatikana”.
Bwn. Lyamuya alikiri uwepo wa changamoto
mbalimbali zilizopo katika taaluma ya upimaji na kutaja baadhi ya
maazimio yaliyoazimiwa katika Kongamano la wapima lililofanyika tarehe 2
na 3 Novemba 2016. Baadhi ya maazimio hayo ni pamoja na kila Kampuni
inayotambulika na kusajiliwa kushiriki kikamilifu katika kuchangia lengo
la kutoa hati laki 4 kwa mwaka 2016/17 kwa kuwasilisha taarifa ya kiasi
cha vipande vya ardhi iliyopima na kila kampuni kwenye mkutano ujao na
kuandaa mapendekezo ya ada ya kitaaluma na gharama za upimaji wa ardhi
zitakazotozwa ambazo zitasambazwa na kutumika nchini kote
Aidha, azimio jingine lililoazimiwa na
wanataaluma hao ni pamoja na kumtambua Waziri wa ardhi, nyumba na
maendeleo ya makazi; Mh. William Lukuvi, kupewa uanachama wa heshima wa
IST/ Institute of Surveyers Tanzania, kutokana na jitihada zake
kubwa katika kushughulikia matatizo ya ardhi nchini, na mchango wake
katika kuwatambua wapima ardhi kuwa ndio suluhisho la kuwawezesha
wananchi kumilikishwa ardhi.
Habari na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
No comments:
Post a Comment