Wednesday, 19 October 2016

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepokea msaada wa mabati 100

gabo01
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemshukuru Mbunge wa Viti Maluum CCM Mkoa wa Lindi Amida Abdalah kwa kuchangia mabati miamoja kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya wazazi katika Hospitali ya wilaya  ya Ruangwa katikati ni  mke wa Waziri Mkuu Mama Mary Majaliwa  na kulia  ni mganga mkuu wa wilaya ya Ruangwa Dr Japhet  Simeo makabidhiano hayo yamefanyika katika Hospitali Ruangwa
Picha na Chris Mfinanga
gabo1
Mama Majaliwa akiwasalimia wauguzi na wananchi walio jitokeza katika makabiano ya mabati miamoja yaliyo tolewa na Mbunge wa Viti Maalumu mkoa wa Lindi
gabo3
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa ameongozana na Mkuu wa mkoa wa Lindi Godfrey Zambi na Mganga mkuu wa Hospitali ya Ruangwa Dr Japhet Simeo wakati waziri mkuu alipotembelea Hospitali ya Wilaya Ruangwa Mkoa wa Lindi

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepokea msaada wa mabati 100 yenye thamani ya zaidi ya sh. milioni mbili kutoka kwa Mbunge wa Viti maalum mkoa  wa Lindi Mhe. Hamida Abdallah.
Msaada huo umetolewa leo (Jumatano, Oktoba 19, 2016) katika hospitali ya wilaya ya Ruangwa wakati wa ziara  ya Waziri Mkuu hospitalini hapo.
Mbunge huyo amesema amekabidhi msaada huo ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa mwezi Aprili mwaka huu wakati Waziri Mkuu alipofanya ziara katika Hospitali hiyo.
“Ulipofanya ziara ya mwezi wanne hospitalini hapa nilikuahidi kukupa mabati  100 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya wanawake. Nilitoa ahadi hii baada ya kuona jitihada kubwa unazozifanya katika kuimarisha hospitali hii,” amesema.
Akipokea msaada huo Waziri Mkuu amemshukuru Mhe. Hamida kwa kutekeleza ahadi yake na kumuomba aendelee kuisaidia hospitali hiyo pindi anapopata nafasi.” Nashukuru sana kwa msaada wako tunajua kutoa ni moyo na si utajiri,”.
Wakati huo huo Waziri Mkuu amesema mkakati wake kwa sasa ni kuboresha huduma za afya kwa kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na zahanati ili kuwawezesha wananchi kupata matibabu karibu na makazi yao.
“Nataka sekta ya afya inapata mafanikio makubwa. Nitashirikiana na wananchi  kuhakikisha kunakuwa na zahanati katika kila kijiji na vituo vya afya kwenye kata zote,” amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Bw. Andrea Chezue alimshukuru Waziri Mkuu kwa jitihada zake za kuboresha huduma hospitalini hapo.
Amesema hivi karibuni walipokea sh. milioni 100 kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Lindi kwa ajili ya ukarabati wa wodi mbili ambazo tayari ukarabati huo umekamilika na zitaanza kutumika kuanzia Novemba 15 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment