Thursday, 5 May 2016

Tundu Lissu:Rais Magufuli awatumbue Majipu Wanasheria Walioshindwa Kumshauri kufuata sheria ya Kukasimisha Mamlaka


 
Rais John Magufuli ametakiwa kutumbua majipu ya wanasheria Walioshindwa kumshauri kufuata sheria ya kukasimisha mamlaka ya Kiuwaziri kwa mawaziri walioteuliwa miezi sita iliyopita.
 
Tundu Lissu amesema hayo Dodoma wakati akitoa maoni kuhusu Mpango Na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya wizara ya Sheria na Katiba kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017, Bungeni mjini Dodoma.

“Kwa kuangalia mifano ya matangazo mbalimbali ambayo yametolewa na watangulizi wa Rais Magufuli tangu sheria ya utekelezwaji wa majukumu ya Kiuwaziri ilipotungwa mwaka 1980, hata mwanafunzi wa sheria wa mwaka Wa kwanza angeweza kumtengenezea draft ya Tangazo la aina hiyo,” Amesema Lissu.

Ameongeza “iweje watu wenye Shahada za uzamivu na uzamili katika sheria washindwe kufanya hivyo kwa karibu ya nusu mwaka tangu wateuliwe? Kama ni majipu ya kutumbuliwa na Magufuli, basi wasomi hawa wa sheria Ni majipu na wanastahili kutumbuliwa.”

“Kwa sababu Rais Magufuli sio mwanasheria, amemteua Mwansheria Mkuu Wa Serikali ambaye kwa mujibu wa ibara ya 59(3) ya katiba ndiye mshauri wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano juu ya mambo yote ya kisheria,” Amesema Lissu.

Kwa sababu hiyo, Rais Magufuli amemteua Dk. Harrison Mwakyembe kuwa Waziri wa Katiba na Sheria ili awe mshauri wake mkuu katika utekelezaji wa Madaraka yake katika masuala ya kikatiba na kisheria kwa mujibu wa ibara 54(3).

“Kwa bahati nzuri Rais amewateua Dk Harrison Mwayembe, Dk Sifuni Mchome, na Amon Mpanju kuwa viongozi wa Wizara ya Katiba na Sheria Ambao wote wasomi wabobezi wa sheria,” amesema.

Amehoji kuwa “Kambi ya Upinzani ianataka kupata majibu sahihi ni kwa nini Wanasheria wabobezi wote hawa wameshindwa kumshauri Rais Magufuli Kutoa tangazo la kukasimisha majukumu ya kiuwaziri kwa mawaziri Mbalimbali aliowateua miezi sita iliyopita?”

Amesema kila mtu anafahamu kwamba Rais sio mwanasheria lakini kutokuwa mwanasheria haimaanishi kuwa juu ya sheria bali anapaswa kufuata sheria za nchi.

Lissu amesema, maana na athari ya kisheria ya kutokuwepo kwa tangazo la Ukasimishaji wa majukumu ya kiuwaziri ni kubwa kutokana na kwamba Mawaziri walioteuliwa wamefanya mambo makubwa mengi ambayo Yalikuwa kinyume cha sheria.

No comments:

Post a Comment