Baadhi
ya vyombo vya habari vimekuwa vinatoa taarifa potofu kuhusu mchakato wa
Mwenyekiti wa sasa wa CCM Dkt. Jakaya Kikwete kukabidhi kijiti cha
uongozi wa CCM kwa Rais John Pombe Magufuli kama ilivyo mila na desturi
ya Chama Cha Mapinduzi.
Yamekuwepo madai eti Mwenyekiti amekataa au anachelewesha kukabidhi kijiti.
Habari hiyo sio kweli kabisa na
ni kinyume chake, kwani Dkt. Kikwete amekuwa akisisitiza kukabidhi
madaraka mapema iwezekanavyo. Kwa ajili hiyo kwenye kikao cha Mei 3,
2016 alikataa kusiongezwe agenda nyingine ambazo zitalazimisha Mkutano
Mkuu Maalum kuchelewa kufanyika kwa sababu ya kukamilisha maandalizi ya
agenda hizo. Alisisitiza agenda iwe moja tu.
Dhamira ya kufanyika Mkutano Mkuu
maalum mwezi Juni, 2016 iko pale pale. Kilichoelezwa kwenye kikao ni
kutaka kukamilisha utaratibu wa kupata fedha za kugharamia mkutano huo.
Taratibu zikikamilika tarehe itapangwa. Mipango ya kutafuta pesa
inaendelea na ikikamilika tarehe itatangazwa.
Tunawataka wana-CCM wasihamanike
wala kubabaishwa na taarifa za upotoshaji zinazofanywa na watu wenye nia
mbaya na CCM. Hawa ni wale wale ambao wamekuwa wakiiombea mabaya CCM
bila ya mafanikio.
Pia tunapenda kukanusha madai ati
kuwa Mwenyekiti Kikwete aliwatahadharisha Wajumbe wa Kamati Kuu kuhusu
ukimya wa Ndugu Edward Lowassa. Hakuna wakati wowote kauli kama hiyo
aliitoa. Ni uzushi mtupu. Jina la Ndugu Lowassa halikutajwa kabisa.
Aidha, tunapenda kukanusha madai
ya kufanyika mkutano baina ya Mwenyekiti wa CCM, Rais wa Jamhuri ya
Muungano, Makamu wa Rais na Katibu Mkuu wa CCM kuhusu uchaguzi wa Katibu
wa Kamati ya Wabunge wa CCM. Hapajawahi kufanyika mkutano wa aina hiyo
siku yoyote na mahali popote. Hivyo madai ya kuwepo kwa tofauti baina ya
Viongozi wakuu kuhusu nani achaguliwe kuwa Katibu wa Wabunge wa CCM
hayana msingi wowote.
Kamati Kuu iliteua Wabunge wanne
kugombea na kuwaachia Wabunge wa CCM kuamua. Kuhusisha Viongozi na hasa
kuzua kuwepo kutokuelewana ni jambo la kusikitisha. Ni taarifa ya uongo
yenye nia ovu kwa CCM na Viongozi wake.
Tunapenda kuwatahadharisha
waandishi wa habari kuandika habari za ukweli. Waache kuzua mambo yenye
kupandikiza chuki na mgawanyiko usiostahili kuwepo ndani ya CCM na
kuyaeneza kwa watu. Waheshimu maadili ya kazi zao.
Napenda kuwahakikishia na kusisitiza kuwa hakuna mgogoro wa kukabidhi kijiti cha uenyekiti katika CCM na wala hautakuwepo.
Imetolewa na;
Ndugu Christopher Ole Sendeka
MSEMAJI WA CCM
MJUMBE WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA,
MJUMBE WA HALMASHAURI KUU YA TAIFA,
05/05/2016
No comments:
Post a Comment