Friday, 6 May 2016

Azam Yaelekea Mkoani Mwanza Kuifuata Kagera Sugar Utakaochezwa Uwanja wa Kambarage Shinyanga


 

Na Tabu Mullah

Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, inatarajia kuondoka mchana huu kuelekea mkoani Mwanza kwa ajili ya kupambana na Kagera Sugar kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Kikosi hicho kikiwasili mkoani Mwanza kinatarajia kufanya mazoezi katika Uwanja wa CCM Kirumba kesho saa 2.00 asubuhi kabla ya mchana kuanza safari ya kuelekea Shinyanga kwa Ajili ya kukabiliana na Kagera Suhara, ambayo inapambana kutoshuka daraja.

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare mbili mfululizo Dhidi ya Simba (0-0) na JKT Ruvu (2-2), ambapo imepanga kufuta makosa kwa kupata Ushindi dhidi ya wapinzani wao hao.

Hall ajiwekea malengo
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz  mara baada ya mazoezi ya leo Asubuhi, Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall, alisema kuwa mipango aliyojiwekea ni kushinda mechi zote tatu zilizobakia kuanzia wa Kagera Sugar, African Sports (Mei 15, Mkwakwani) na Mgambo JKT (Mei 21, Azam Complex).

“Najua mechi hizo zitakuwa ngumu kutokana na kucheza na timu zinazopigania kutoshuka Daraja, tumejipanga na mechi mbili dhidi ya Sports na Kagera tutakazochezea kwenye Viwanja vibovu, tutacheza kwa staili yetu ya kutumia mipira ya juu na kupeleka mipira mbele ili kupambana na hali ya viwanja hivyo,” alisema.

Katika hatua nyingine Hall alisema kuwa moja ya malengo yake mengine yaliyobakia ni kuipa Ubingwa wa Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) timu hiyo baada ya kuingia fainali itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Mei 28 mwaka huu dhidi ya Yanga.

“Tulianza msimu kwa kupata Kombe la Kagame, hivyo kupata Kombe la FA itakuwa imetutengenezea rekodi nzuri, hivyo nitahakikisha tunapambana kuweza kutwaa taji hilo,” Alisema.

Azam FC katika mchezo huo wa Jumapili inatarajia kuendelea kuwakosa mabeki Shomari Kapombe, Pascal Wawa, Wazir Salum, viungo Frank Domayo, Jean Mugiraneza, ambao ni Wagonjwa huku Salum Abubakar ‘Sure Boy’ akikosekana baada ya kukusanya kadi tatu za Njano.

Lakini habari njema ni kurejea kwa beki Aggrey Morris aliyemaliza adhabu ya kukosa mchezo Uliopita dhidi ya JKT Ruvu baada ya kukusanya kadi tatu za njano.

Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB kwa sasa inashika nafasi ya tatu kwenye Msimamo ikiwa na pointi 57, nyuma ya Simba inayoshika nafasi ya pili wakiwa na pointi 58 na Mchezo mmoja mkononi huku Yanga inayohitaji pointi tatu ili iwe mabingwa wa msimu huu ikiwa kileleni kwa pointi 68

No comments:

Post a Comment